Diamond kumuoa Zari au Hamisa?

Muktasari:

Mwanamuziki huyo amesema atachagua wa kuoa kati ya wazazi wake wenza hao


Dar es Salaam. Hayawi hayawi sasa yamekua. Kile kilichokuwa kikisubiriwa na mashabiki wa mwanamuziki nyota wa Tanzania, Diamond Platnumz huenda kikatimia hivi karibuni.

Hiyo ni baada ya Diamond kuanika wazi kuwa anatarajia kuoa mwaka huu na atachagua nani wa kuoa kati ya wazazi wenzake, Hamisa Mobeto na Zarina Hassan maarufu kama Zari.

Awali, katika siku ya wanawake duniani Machi 8 mwaka huu, Diamond, aliandika katika ukurasa wake wa Instagram akimtakia mama yake heri ya siku hiyo lakini katika salamu hizo aliahidi kuwa ataoa mwaka huu.

Diamond aliamua pia kutumia nafasi hiyo kumuomba mama yake msamaha kwa makwazo na magumu yote ambayo amekuwa akimpitisha katika mengi ikiwamo katika mitandao ikiwamo kutukanwa.

Ingawa maneno ya Diamond yalikuwa kitendawili kwa sababu hajaweka wazi ni lini au nani anategemea kumuoa mwaka huu, lakini MCL Digital June 18, 2018 lilifanya naye mazungumzo na kumhoji ni nani wa kumuoa katika ya Hamisa na Zari  wanawake aliokwisha zaa nao.

Diamond alisema  atajua baadaye ni nani atamuoa kati ya wazazi wenzake hao wawili.

“Siwezi kumtaja wa kuoa, ila kati ya hao wawili mimi ndio nitajua nani wa kumuoa, Hamisa au Zari, hivyo watu waendelee kusubiria ndoa tu,”alisema.

Aidha kwa upande wa kuwa na msongo wa mawazo kama anavyodaiwa na dada yake amekana kuwa hivyo na amesema hana tabia ya kuwa na msongo wa mawazo kwenye masuala ya mapenzi.