Diamond ni Lady Jaydee wa kiume

Muktasari:

Njia za Jide anapita Diamond leo, ingawa kapiga hatua nyingi zaidi ya dada yake. 

Stara Thomas ni kama kaondoka, yeye yupo. Unique Sisters walitoweka, yeye yupo. Dataz, Zay B, Sister P, Fina Mango, Klynn, Rah P na warembo kibao kwenye gemu mpaka huyu wa juzi Bibi Cheka katoweka, yeye yupo.

Katikati ya masela. Katikati ya machizi muziki Katikati ya mfumo dume, akatoboa. Haikuwa kazi rahisi. Wakati ule ilikuwa ngumu mwanamuziki wa kuimba kuteka watu. Achilia mbali mtoto wa kike. Toto la Kikurya likapasua kindava.

Alisaidiwa? Sawa, lakini huwezi kusaidia mtu asiyejiweza akaweza. Waliosaidia walijua sehemu ya kupata faida. Kusubiri ashuke ni sawa na mwanamke wa miaka 30 kuendelea kusubiri apate ‘handsome boy’ ili aolewe.

Sauti yake imetumika sana kupamba nyimbo nyingi katika viitikio.

Kwa miaka mingi kwenye muziki alitumia kupambana na soko. Huku kiki yake ikiwa kulilia mapenzi.

Mpaka Ndindindi ya juzi unagundua Jide aligeuza biashara kutendwa kwake kimapenzi.

Hakuna alichobakisha Jide kwenye muziki ila kuna kitu muziki umebakisha kwa Jide. Anastahili heshima. Bahati mbaya Wabongo tulishatoa talaka ya heshima. Hatuna heshima panapostahili heshima.

Wanamuziki wengi wa kike na wa kiume wametoweka kwenye muziki. Jide bado yupo na misukosuko yake. Anakomaa kivyake. Mambo mengine tuache kusubiri mtu atangulie mbele ya haki ndipo tuangushe mamilioni ya sifa.

Kama vijana wanajiingiza kwenye matumizi ya dawa za kulevya kwa sababu ya ugumu wa maisha. Jide tungeshamzika kwa matumizi ya dawa za kulevya kwa ugumu wa mapenzi.

Jide, ugumu wa penzi aligeuza pesa. Stress za mapenzi zikatunga msululu wa pesa kwenye akaunti yake. Mr Nice hakukosea katika maisha yake. Kufulia kwake ilikuwa makusudi ya Mungu ili kuwasaidia kina Ommy Dimpoz ambao leo wanakumbuka kuwekeza.

Jide uwepo wake ni makusudi ya Mungu ili Nandy na Ruby kama siyo Malkia Karen, wajue muziki ni maisha siyo lazima usubiri uteuzi wa Rais kama Jokate Mwogelo. Jide anastahili heshima kubwa zaidi ya kuitwa Komandoo.

Kama ilivyo kwa Jide. Diamond naye amekuwa alitumia matukio yake mengi ya kimapenzi kugeuza pesa. Kiki zake ni mapenzi hata nyimbo zake nyingi ni mapenzi tupu. Zaidi ya muziki kitu pekee anachoongelewa na mashabiki ni matukio ya mapenzi.

Naye wakati anatoka kimuziki kulikuwa na kundi na machizi muziki. Wakati Jide anatoka wanamuziki wengi walikuwa wa kiume, yeye ametoka kukiwa na wanamuziki wengi wa kike na wa kiume.

Wakati Jide alipambana kutengeneza soko lililotekwa na wanaume, Diamond alipambana kipindi ambacho bila pesa huwezi kupasua anga. Ndiyo maana kina Papaa Misifa wakatia mzigo wa maana ili dogo atoke.

Zamani ilikuwa ukitoa muziki mzuri lazima ubambe. Diamond alitoka kipindi ambacho hata wimbo uwe mzuri vipi kama hujawekeza mkwanja wa promo utaishia kusikiliza ghetto na dem wako. Dogo akatoboa katikati ya mkwanja mbele.

Kwa sasa yupo kwenye kilele cha Mlima Kilimanjaro. Anatazama wenzake kwenye viunga vya mji wa Moshi. Game liko chini ya soksi zake. Analiendesha na linamtii.

Anajituma. Ana pesa. Ni maarufu na anapendwa. Unaweza kuwa maarufu usipendwe. Hata shetani ni maarufu lakini hapendwi. Na unaweza kuwa na pesa na usiwe maarufu. Kuna matajiri kibao wakipita Kariakoo hakuna anayewatazama.

Hakuna uchawi kama kujituma na kujitambua. Diamond anavyo vyote hivyo. Moja kati ya akili mbovu tuliyonayo ni kutopenda mtu mmoja awe juu kila siku. Tunataka kuona mtu anapanda na kushuka.

Furaha ya Waswahili ni kuzalisha Mr Nice na Ferouz mwingine. Tunakerwa kuona Diamond anapaa kila siku. Furaha yetu ni kuona anapaa juu na kushuka chini ghafla.

Hasira za kutopenda hilo tunalihamishia katika kutafuta mtu wa kumfunika. Wabongo wanalazimisha upinzani kwake. Apatikane mtu wa kuwa juu ya Diamond.

Wanakerwa na umaarufu wake. Mafanikio yake. Na hata uwepo wake duniani. Sasa wenye mioyo hiyo ya kipuuzi wanatulazimisha tuamini kuwa hana mashairi mazuri kama zamani wakati anaanza muziki.

Walimpenda Cabo Snoop wa Parakatatumba, bila kuelewa lugha yake wala ubora wa sauti yake. Makhirikhiri walibamba bila kuelewa lugha yao. Huu siyo wakati wa nyimbo kama Mbagala au Nitarejea.

Watu wanataka fleva tu. Sauti? Davido hafikii hata robo ya sauti ya Barnaba. Nani mwenye mafanikio na umaarufu kati yao? Daraja la Diamond siyo la kuimba shida za Yombo. Ni midundo mizuri na mtiririko mtamu wa maneno ili hata asiyeelewa lugha basi afurahie.

Uwekezaji wa Jide ulikuwa wa wazi na mkubwa wakati wenzake pesa nyingi ziliishia kwenye kaunta za Mbowe pale Billcanas. Pia Diamond uwekezaji wake unaeleweka na ni mkubwa huku wenzake wakiishia kutukanana mitandaoni.

Licha ya muziki hivi sasa kuonekana unapaa kimataifa. Ukweli ni kwamba mwanamuziki mmoja ndiye anayepaa huku wenzake wakiwa palepale. Hatuwezi kuwa na staa mmoja wa muziki miaka nane halafu tuseme muziki unapanda.

Kama utafuatilia ni Diamond pekee na wanaomzunguka wenye uhakika wa shoo kila wiki. Wengine wengi wanasubiri msimu wa Fiesta. Hivi sasa nyimbo nyingi zitatolewa kwa sababu Fiesta inajongea.

Wakati ule licha ya uwepo wa wanamuziki wa kike lakini Jide ndiye aliyekuwa anatamba zaidi. Kuanzia tuzo mpaka kwenye shoo za ndani na nje ya nchi. Na kushirikishwa na wanamuziki wa kimataifa. Wenzake wakatoweka mazima.

Leo licha ya uwepo wa wanamuziki wengi lakini muda mwingi tunamsikia Diamond tu kwenye tuzo na shoo nyingi za ndani na nje ya nchi. Pamoja na kushirikishwa na nyota wa kimataifa. Kwa mwendo huu wapo watakaoamua kushika jembe badala ya maiki.

Njia za Jide anapita Diamond leo, ingawa kapiga hatua nyingi zaidi ya dada yake. Jide aliishia bara la Afrika, dogo kavuka bahari ya Atlantic mpaka kwenye vibaraza vya mama zao kina Ricky Ross.