Thursday, January 11, 2018

Diwani Chadema aeleza sababu wenzake kuhama

 

By Geofrey Nyang’oro, Mwananchi gnyangoro@mwananchi.co.tz

Diwani Kata ya Mivinjeni (Chadema), Frank Nyalusi amesema chanzo cha madiwani wanane wa chama hicho mkoani hapa kujiuzulu ni mgogoro uliotokana na uchaguzi wa naibu meya wa Manispaa ya Iringa uliofanyika mwishoni mwa mwaka jana.

Akizungumza jana, Nyalusi alisema katika uchaguzi huo diwani wa Gangilonga (Chadema), Dadi Igogo alichaguliwa kuwa naibu meya akichukua nafasi iliyoachwa wazi na Joseph Ryata wa Kwakilosa aliyemaliza muda wake.

“Mimi niseme tu kilichosababisha madiwani kuondoka ndani ya chama ni uchaguzi wa naibu meya, katika uchaguzi ule chama kiliteleza kidogo,” alisema.

“Madiwani tulikaa na kukubaliana kuwa Ryata aendelee na unaibu meya, lakini wengine walifanya mabadiliko na kumuweka Igogo.”

Nyalusi alisema jambo hilo lilichangiwa na baadhi ya madiwani kuwa na wivu wa madaraka huku akitolea mfano jinsi alivyoondolewa katika nafasi ya mwenyekiti wa wilaya.

“Nilihoji na kusema kwa kuwa naibu meya amefanya vizuri aendelee kwa sababu vyama vya upinzani huingiziwa matatizo kipindi cha uchaguzi,” alisema diwani huyo.

“Binafsi sikujiuzulu udiwani, tulikaa kwenye vikao na kukubaliana kumaliza mgogoro. Dhambi waliyobaki nayo madiwani waliojiuzulu ni kukosa uvumilivu.”

Akizungumzia kauli ya Nyalusi, Katibu mwenezi wa CCM Wilaya ya Iringa mjini, Edo Bashiru alisema hoja yake imejibu jambo linalojadiliwa na baadhi ya watu kwamba wanaokwenda CCM wamenunuliwa.

“Baada ya mwenyekiti wao kusema tatizo lao lilikuwa migogoro ya ndani, kazi ya kujibu hoja hiyo imekuwa nyepesi. Tunawaomba wananchi waachane na siasa hizi za uongo na waiamini CCM,” alisisitiza Bashiru.

Katibu huyo aliongeza kuwa CCM inawakaribisha madiwani wote wa Chadema, lakini akasisitiza kwamba hawatawachukua wale wasioweza kufanya kazi.

Mkazi wa Iringa, Matwew Kakitumbe aliwataka wanasiasa kuheshimu viapo wanavyoapa kwa kuwa uamuzi wa kuhama vyama ni kutotimiza matakwa ya viapo hivyo.

Joshua Maleko aliutaja ulafi wa madaraka kuwa unaliingiza Taifa katika migogoro ya kisiasa na kuwatwisha mzigo mkubwa wananchi ambao wanalazimika kujikamua kugharimia chaguzi ndogo zinazofanyika.     

-->