Diwani wa CCM atuhumiwa kumpigia kura wa Chadema

Muktasari:

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake juzi, Katibu wa CCM Wilaya ya Musoma Mjini, Bernard Ghaty alisema hilo lilitokea Agosti 10 katika kikao cha uchaguzi uliofanyika katika Kata ya Murangi Halmashauri ya Musoma Vijijini.

 Diwani wa CCM Kata ya Suguti, Musoma Mjini Mkoa wa Mara, Denis Ekwabi amekisaliti chama chake baada ya kumpigia kura mgombea wa Chadema wakati wa uchaguzi wa makamu mwenyekiti wa halmashauri.

Madiwani wenzake wamelaani kitendo hicho wakidai hakivumiliki ndani ya chama chao.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake juzi, Katibu wa CCM Wilaya ya Musoma Mjini, Bernard Ghaty alisema hilo lilitokea Agosti 10 katika kikao cha uchaguzi uliofanyika katika Kata ya Murangi Halmashauri ya Musoma Vijijini.

Hata hivyo, Ekwabi alikana kumpigia kura mgombea wa Chadema akisema walikuwa wanataniana na madiwani wengine kwa sababu na yeye alikuwa mgombea.

Halmashauri hiyo ina madiwani 26, kati yao CCM ni 22 na Chadema wanne lakini katika kura zilipopigwa, mgombea wa Chadema alipata kura tano huku wa CCM akipata 21.

Alisema kwa mujibu wakatiba yao ni kosa kubwa kupigia chama kingine na kwamba kukutana na kamati ya maadili ili kutoa uamuzi kuhusu suala hilo kabla ya kamati ya Mkoa kulitolea tamko.

Katibu Msaidizi wa Musoma mjini, Kapis Adogo alisema alichokifanya diwani huyo hakipaswi kuvumilika kwani alifanya maamuzi ya hasira baada ya kushindwa kwenye kura za maoni ambazo zilipigwa ndani ya chama kabla ya uchaguzi huo.