Diwani wa Chadema Musoma, ajiunga na CCM

Muktasari:

  • Mugingi Muhochi alijiunga na Chadema akitokea CCM katika uchaguzi wa mwaka 2015 na kugombea ambapo alishinda udiwani kata ya Kianyari.

Musoma. Diwani wa kata ya Kianyari wilayani Butiama, Mugingi Muhochi (Chadema) amejiuzulu wadhifa wake na kujiunga na CCM.

Akizungumza leo Septemba 11 Muhochi amesema amechukua uamuzi huo baada ya kuridhishwa na utekelezaji wa ilani ya CCM chini ya Mwenyekiti wa CCM, Taifa, John Magufuli.

Muhochi ambaye katika Uchaguzi Mkuu uliopita aligombea udiwani kupitia CCM lakini alishindwa katika kura za maoni za chama hicho na kuamua kujiunga na Chadema. Baada ya kujiunga na Chadema, alishinda udiwani kata ya Kianyari.

Muchochi amesema ameamua kurudi CCM kwa hiari yake mwenyewe na bila kushawishiwa na mtu yeyote.

Amesema katika kata yake yenye vitongoji 20 ambavyo vyote viko chini ya CCM amekuwa akipata ushirikiano wa kutosha licha ya tofauti ya vyama.

Akizungumza mara baada ya kumpokea diwani huyo, Katibu wa CCM wilaya ya Butiama, Ashura Suleman amempongeza diwani huyo kwa uamuzi alioufanya.