VIDEO: Dk Bashiru aapa kuwalima barua Spika, Makamu wa Rais Zanzibar

Katibu Mkuu mpya wa CCM, Dk Bashiru Ally akizungumza alipokuwa akifanyiwa mahojiano maalum na waandishi wa gazeti la Mwananchi, ofisini kwake jijini Dodoma juzi. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

Hatua hiyo inakuja baada ya kumlima barua waziri mkuu akimtaka kushughulikia mambo matatu ili chama hicho kiendelee kuaminiwa na wananchi.

Dar es Salaam. Siku chache baada ya katibu mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally kusema amemwandikia barua tatu Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuhusu wajibu wake, mtendaji huyo mkuu wa chama tawala hajapoa; sasa amewataka viongozi wengine wajiandae kulimwa barua iwapo hawatatimiza wajibu wao ipasavyo.

Hatua hiyo inakuja baada ya kumlima barua waziri mkuu akimtaka kushughulikia mambo matatu ili chama hicho kiendelee kuaminiwa na wananchi.

“Waziri Mkuu, tangu nimeingia nimekupiga barua tatu. Moja ya mgogoro wa ardhi wa Chanika (Dar es Salaam), ya ma -DC (wakuu wa wilaya) na RC (wakuu wa mikoa) kutohudhuria vikao vya kamati za siasa, na nyingine ya mipango ya maendeleo kuandikwa kwa Kiingereza wakati inakwenda kwa wakulima na wavuvi.

“Na ujipange zinaweza kufika 100 au 1,000. Tunataka chama kinachokwenda kutatatua matatizo ya wananchi,” alimwambia Waziri Mkuu, Majaliwa mbele ya wabunge wa chama hicho katika hafla ya kumuaga mtangulizi wake, Abdulrahman Kinana na kumkaribisha yeye iliyoandaliwa na wabunge hao mjini Dodoma, Juni 20.

Na kama watendaji wa Serikali walidhani hiyo ndiyo itakuwa mara ya mwisho kwa mtendaji huyo ‘kuwatwanga’ barua anapoona mambo hayaendi kama chama kinavyotaka, basi watakuwa wanakosea.

Sasa amewataka vigogo wengine akiwemo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Spika wa Bunge la Muungano na Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar kujiandaa.

Akizungumza katika mahojiano maalumu na Mwananchi katika ofisi za makao makuu ya CCM jijini Dodoma, Dk Bashiru alisema hataishia kwa Waziri Mkuu peke yake, bali viongozi wengine na watendaji na wapo watakaowajibishwa kwa kutotekeleza ilani ya CCM.

“Siyo tu kwamba nitamlima barua Waziri Mkuu peke yake, yeyote. Wengine nawapigia simu, hizo simu hazihesabiki na ninapata majawabu hapohapo,” alisema Dk Bashiru.

“Kazi kubwa ninayofanya siyo kupiga simu na kulima barua tu, ni kufanya utafiti na kufuatilia ili kubaini kasoro na makosa, na kufuatilia barua zile kama zina majawabu ya kutosha. Kama siridhiki napeleka kwenye vikao ili viamue.”

Huku akisisitiza kuwa huo si utaratibu mpya, Dk Bashiru alisema vikao vyote vya chama vina wajumbe ambao pia ni watendaji wa Serikali na wanasiasa.

“Mimi sijazua jambo jipya hapa. Kazi ya vikao vyote vya chama ngazi zote ni kuisimamia Serikali. Ndiyo maana katika vikao vyote, watumishi wote na baadhi wa Serikali ni wajumbe wa vikao vyetu kwa nafasi zao. Madiwani wana nafasi kwenye vikao, wabunge wana nafasi katika vikao vyetu, wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya wana nafasi katika vikao vyetu,” alisema.

“Kamati Kuu kwa muundo wake, Waziri Mkuu ni mjumbe wa kamati kuu. Haji tu pale kwa sababu ni Waziri Mkuu, aweze kueleza kwenye mkutano, aweze kuhojiwa na Kamati Kuu.

“Spika wa Jamhuri ya Muungano na Spika wa Zanzibar ni wajumbe kikatiba. Si kufurahisha, ni kutaka kuunganisha chama na Serikali ili kuwe na mtazamo wa pamoja.

“Mimi katibu mkuu ni mtendaji mkuu wa vikao hivyo, kwa hiyo ninapomwandikia Waziri Mkuu au Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar natimiza wajibu wangu kikatiba na taratibu zilizopo.”

Tofauti na mtangulizi wake, Kinana aliyekuwa akitaja mawaziri na watendaji wa Serikali kuwa mizigo wakati wa Serikali ya Awamu ya Nne, Bashiru amesema hatakuwa akilalamika majukwaani, bali wasiotekeleza wajibu wao watawajibishwa na vikao.

“Mimi nasema wapo watu watawajibishwa na vikao vya chama na hilo si jambo jipya. Kwa hiyo mimi siwezi kulalamika wakati niko kwenye chama. Au kupita kutangaza majukwaani wewe waziri hufanyi hivi, hata kidogo.”

Mali za chama

Kuhusu mali za CCM, Dk Bashiru aliyeongoza tume ya kufuatilia mali hizo kwa miezi sita, alisema ndilo jambo kubwa alilolikuta kwenye chama hicho akisisitiza kuwa amekuta hali ni mbaya.

“Hili ndilo nimelikuta kubwa sana na ndiyo sababu ya tume niliyoiongoza ya kuhakiki mali za chama,” alisema.

Alisema tume yake ililenga kuhakikisha mali zote za chama zinatambuliwa, ziko wapi, kiasi chake, zina hali gani na zinasimamiwaje.

Pia alikuwa na wajibu wa kujua zipi zipo salama, zilizoibiwa na ni utaratibu gani watafanya ziweze kuwa na mchango katika kuwezesha chama kujitegemea kiuchumi.

“Unajua wewe ni Mtanzania, unajua hali yetu ya usimamizi ilivyo na unajua mambo yanavyoendelea hata kwenye Serikali, ukiwa mkweli ndivyo mambo yalivyo hata kwenye chama,” alisema.

Alisema katika utafiti wao walibaini mambo makubwa matatu ambayo ni pamoja na kiwango kidogo cha maarifa ya usimamizi wa mali za chama na mapendekezo yaliyotolewa ni kuwapa utaalamu watendaji.

“Tatizo la pili kulikuwa na aina fulani ya udokozi wa mali, wakati mwingine taratibu zilikuwa hazifuatwi, wakati mwingine mali zina thamani kubwa lakini mchango wake ni mdogo, wakati mwingine ni mikataba ya watu ambao pengine tumeingia nao tuwe na ushirikiano. Kumekuwa na tatizo,” alisema Dk Bashiru.

Alisema yeye kama mtendaji na msimamizi mkuu wa mali za chama hicho atahakikisha mapendekezo yao yanafuatwa ikiwa ni pamoja na kuwawajibisha watendaji waliokutwa na hatia.

“Kwa hiyo sina shaka wale wote ambao walipaswa kuwajibika na hawakuwajibika, utaratibu upo watawajibika. Sasa watu ni akina nani hayo majina, mali hazisimamiwi na hewa kuna watu sasa wale waliosimamia vizuri watapongezwa, na wale watakaoonekana kuwa wamelegalega wanaweza kuwekewa utaratibu wa kuwajibishwa au kuwekewa utaratibu wa kuwaongezea maarifa.”

Mbali na kuwawajibisha watendaji hao, alisema sehemu kubwa ya watendaji wataongezewa uwezo ndani ya chama na maarifa ya usimamizi wa mali za chama.

“Kwa sababu tuna rasilimali watu kubwa, una watu kama 1,000 wanahitaji kulipwa kila mwezi, tuna vitendea kazi kama magari, majengo yanayohitaji kuhifadhiwa na kusimamiwa na yote yanahitaji maarifa na mbinu.”

Siasa za majukwaani

Kuhusu siasa za majukwaani, Dk Bashiru alisema mtindo huo si kipimo cha utendaji wake, bali atazitumia pale itakapohitajika.

“Siwezi kupimwa na idadi ya mikutano niliyoifanya au na sauti kubwa niliyoipaza na saa niliyokuwa jukwaani. Niongee nini? Natoa taarifa jukwaani au nafafanua masuala jukwaani au najibu hoja za wananchi jukwaani. Jukwaa lipi? Jukwaa la kupiga porojo?” alihoji.

Alisema kabla ya kwenda jukwaani analiandaa kwani wanaosumbuliwa na majukwaa ni wanasiasa wa kuchaguliwa na siyo wa kuteuliwa.

“Lile jukwaa hasa ambao wasipokwenda jukwaani wanapunguza siasa zao ni wanasiasa wa kuchaguliwa kwa kura, sisi tulioteuliwa kwa barua ya ajira na tunalipwa mishahara, mimi nalipwa. Hao wengine wanapata posho na kujitolea. Mimi sijitolei, hii ni ajira. Nafuata masharti ya ajira hii, huko kwenye Katiba kwa mimi na watendaji wangu.”