Sunday, June 3, 2018

Dk Bashiru na mjadala mpya wa watendaji wa vyama majukwaani

 

By Tausi Mbowe, Mwananchi tmbowe@mwananchi.co.tz

Mjadala mkubwa wa kisiasa kwa wiki nzima ulikuwa ni mabadiliko ya uongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) hasa kwa nafasi ya katibu mkuu, baada ya Abdulrahman Kinana kung’atuka na kukabidhi mikoba hiyo kwa Dk Bashiru Ally.

Kinana aliomba kupumzika na kikao cha Halmashauri Kuu Taifa ya chama hicho (NEC) kilichoketi mapema wiki hii chini ya uenyekiti wa Rais John Magufuli kikaidhinisha ombi hilo na kufanya uteuzi wa mtendaji mpya.

Tangu Kinana alipoteuliwa mwaka 2012, utendaji wake ulimfanya kuonekana kuwa ni mwanasiasa wa kipekee baada ya kutumia muda mwingi akizunguka nchi nzima majukwaani akikinadi chama hicho.

Kutokana na utendaji huo, Kinana (66) anaelezwa na makada kuwa ulikirejeshea chama uhai baada ya kuwa kimezidiwa na ‘makombora’ ya wapinzani.

Hata pale Kinana alipoamua kukaa kimya na kutoonekana majukwaani kutokana na sababu mbalimbali, hali hiyo ilionekana wazi na kuzua minpng’ono kwa kuwa matarajio ya wengi yalikuwa kwamba kiongozi wa aina yake lazima aonekane majukwaani.

Kwa kufuatilia mwenendo huo wa Kinana na pengine hata watangulizi wake, ndio maana kauli ya Dk Bashiru kwamba yeye hataonekana majukwaani inatazamwa mno kwa jicho la kisiasa na kuibua mjadala.

Dk Bashiru mbali na kujisemea yeye kwamba yeye si mtu wa majukwaani, ameongeza kuwa ni marufuku hata kwa watendaji wengine wa chama hicho kupiga siasa za majukwaani, bali waachie viongozi waliochaguliwa kwa ajili ya kazi hiyo kama wenyeviti na makatibu waenezi.

“Siasa za majukwaani ni za mwenyekiti wa chama akisaidiwa na makamu wenyeviti wake wawili. Kule mikoani kuna wenyeviti wa vyama wa mikoa, wa wilaya, kuna wabunge na madiwani,” alinukuliwa Dk Bashiru siku ambayo alikabidhiwa ofisi na mtangulizi wake.

Msimamo huu ni kinyume na mazoea ya kisiasa ndani na nje ya chama hicho, hivyo huenda kiongozi huo amekuja na mtindo mpya ambao ama unaweza kuisaidia au kuiponza CCM.

Mbali na CCM ambacho ni chama tawala wapinzani, mtindo huo mpya unaweza kuwa na maana kubwa kwa vyama vya upinzani ambao kwa namna moja au nyingine vimekuwa vinaiga utendaji wa CCM au vinabuni mbinu mpya kwa kuukosoa utaratibu wa chama tawala.

Wachambuzi wa masuala ya siasa wanaufananisha uamuzi huo wa Dk Bashiru sawa na kuteleza, kwamba hakupaswa kutoa kauli hiyo katika kipindi hiki ambacho bado hajajua mahitaji halisi ya wanachama wake.

Wakati wasomi wakisema kuwa kauli hiyo ni ngeni katika siasa, wapinzani wa CCM, hasa Chadema, wanasema kauli hiyo imekaa vibaya kwa kuwa si rahisi kumtofautisha katibu mkuu wa chama cha siasa na mwanasiasa.

Wanasiasa, wasomi watoa maoni

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Iringa (UoI), Dk Jimson Sanga anasema kauli ya katibu mkuu huyo ni mawazo mkanganyiko.

“Ni kauli mpya, haijazoeleka ndani ya chama, pengine tumpe muda tutaelewa lakini kwa kweli inaleta mkanganyiko sana,” anasisitiza Dk Sanga.

Kwa mujibu wa Dk Sanga, pengine katibu mkuu huyo ameamua kutoa kauli hiyo kutokana na kuakisi kile mwenyekiti wake wa chama, Dk Magufuli anachokitaka.

“Sote ni mashahidi, mwenyekiti wa chama chake taifa mara kadhaa amekuwa akitaka watendaji wasijihusishe na masuala ya siasa na badala yake wafanye kazi ya kuisimamia Serikali, lakini pia kuna hili la kutoshiriki siasa mpaka mwaka 2020 pengine hilo pia ameliona,” anaongeza Dk Sanga.

Dk Sanga anasema kauli ya Dk Bashiru ni dhana inayohitaji ufafanuzi kwa kuwa katibu mkuu ndiye mtendaji wa chama, anatakiwa kuhakikisha kinakuwa imara na kushika dola.

“Tumpe muda hii kauli inahitaji ufafanuzi, lakini pia ni kauli ambayo haijazoeleka katika medani za siasa wala chama, hivyo si rahisi kuichambua,” anasema.

Wakati Dk Sanga akisema hayo waziri wa zamani wa Serikali ya awamu ya tatu, Njelu Kasaka anasema anavyoelewa yeye katibu mkuu wa chama chochote cha siasa ni mwanasiasa.

“Huwezi kujiondoa katika siasa wakati wewe ni mtendaji mkuu wa chama cha siasa ambacho kazi yake kubwa ni kufanya siasa,” anasisitiza Kasaka.

Kwa mujibu wa waziri huyo wa zamani, kuna wakati ni lazima kiongozi huyo hataweza kukwepa kupanda katika majukwaa, hasa kipindi cha uchaguzi, ili kuwasaidia wanasiasa wake, hivyo mazingira hayo yatamlazimu kufanya hivyo.

Hata hivyo, Kasaka anasema anakubaliana na katibu mkuu huyo kwamba watendaji wa kada nyingine kama wahasibu na walinzi ni sawa kukaa ofisini kutekeleza kazi za kiutendaji, lakini kwake yeye hilo haliwezekani.

“Katika chama huwezi kuwaondoa katika majukwaa mtu kama katibu mkuu, msaidizi wake na katibu wa itikadi na uenezi. Hawa kimsingi ni wanasiasa na nafasi zao ni za kisiasa zaidi kuliko utendaji,” anaongeza Kasaka.

Kasaka anasema kauli hiyo haina tija kisiasa ingawa hawezi kufanana na wanasiasa wa kuchaguliwa.

“Hawezi kumfikia diwani au mbunge lakini na yeye anapaswa kukijua chama kuanzia chini na hawezi kukaa ofisini tu amejifungia akategemea atajua kila kitu; yapo mazingira ambayo yatamlazimisha kutoka, hivyo ajiandae tu,” anasema.

Dk Mashinji atoa neno

Kwa upande wa Katibu Mkuu Chadema, Dk Vincent Mashinji anasema kauli hiyo imekaa vibaya kisiasa.

Kwa mujibu wa Dk Mashinji ambaye naye aliteuliwa akitokea katika taaluma akiwa daktari wa binadamu, vyama vya siasa vina mambo makuu matatu.

“Katika mambo hayo ambayo ni kujitawala, kutawala na kujitangaza, kila moja lina umuhimu wake na hapa anachotwambia Dk Bashiru ni kwamba katika uongozi wake yeye hatajitangaza.

“Huwezi kufanya siasa bila kujitangaza, leo hii kampuni ya vinywaji licha ya kukaa katika soko kwa miongo mingi bado inaona umuhimu wa kupitisha magari barabarani na kuelezea ubora wa bidhaa zao; ‘how can you run a political part’ (ni kwa jinsi gani unaweza kuendesha chama cha siasa) bila kujitangaza? anahoji Dk Mashinji.

Dk Mashinji anamtaka kiongozi huyo atafakari upya kauli yake kwani haina mashiko katika ulimwengu wa siasa.

“Kwani kazi ya vyama vya siasa ni nini? Hata sheria ya vyama vya siasa ya mwaka 1992 inasema wazi kuwa kazi ya vyama vya siasa ni kutoa maoni kuhusiana na Serikali, sasa hayo maoni kama hupandi jukwaani utayatolea wapi, chumbani?” anahoji Dk Mashinji.

Anasema pia kuwa sheria hiyohiyo inaruhusu wanasiasa kujinadi kwa wanachama wake ili kutekeleza majukumu yao na kumshangaa katibu mkuu wa CCM kwamba kwa kuamua kukaa kwake ndani kama mtendaji tu atajinadi vipi?

Anasema kwa kauli hiyo, katibu kuu huyo amejipambanua kwamba yeye ni kipaza sauti cha mwenyekiti ambaye mara zote amekuwa akikemea siasa za majukwaani mpaka ifikapo uchaguzi mkuu wa 2020.

Hata hivyo, Dk Mashinji anasema kuwa pengine kiongozi huyo ameona hana majibu ya kuwapa wananchi pindi atakapopanda jukwaani kunadi sera za chama chake, ndiyo maana akaona atulie ofisini na kuwapiga marufuku watendaji wake.

“Hawa ndugu zetu sasa hawana majibu, wameahidi vitu vingi lakini hawajavitekeleza, mfano mzuri ni Sh50 milioni walizoziahidi kutoa katika kila kijiji ziko wapi? anahoji Dk Mashinji.

“Kutokana na hilo na mengine mengi wanaona ni bora kukaa kimya japo si muarubaini’ dawa ni kutekeleza ahadi ili awe huru,” anasisitiza.

Dk Mashiniji anasema mwenzake Dk, Bashiru ni msomi mzuri hakupaswa kutoa majibu mepesi na hivyo amewahi sana kutoa kauli hiyo bila kukisoma chama ili kujua aanze wapi.

Dk Mashinji alienda mbali zaidi kwa kupinga watu wanaomfananisha yeye na katibu mkuu huyo mpya, na kusema kamwe hawezi kufanana naye kwa kuwa yeye anasimamia anachokiamini.

“Siwezi kufanana naye kabisa; kwanza sibadiliki lakini kwake hili limekuwa tofauti tumeshuhudia ameshabadilika. Awali msimamo wake katika Katiba ulikuwa tofauti, lakini baada ya kupata madaraka tu sasa anazungumza lugha nyingine.”

Dk Mashinji anasema kinachopaswa kwa kiongozi huyo ni kuhakikisha anakuwa na utulivu katika uongozi, kuchuja maneno na kusikiliza wengine; “Kama kiongozi alipaswa kusubiri kwanza kutoa kauli ile akajifunza siasa zinakuaje. Ni mara kumi kunyamaza kuliko kuchanganya watu wako.

“Jambo lingine ni lazima ajue kwamba silaha yake ni ulimi wake, hivyo akiutumia vizuri utaleta manufaa lakini akiutumia vibaya utamcheka.

Alichokisema Dk Bashiru

Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa ofisi Dk Bashiru alisema kazi yake si mwanasiasa na kwamba katika kipindi chake hatajihusisha na siasa za majukwaani.

“Ni marufuku kwa watendaji kufanya kazi ya siasa. Kazi ya siasa safi ni wale waliochaguliwa kwa miaka mitano. Sisi ni watendaji, naweza nikakaa nusu saa, naweza nikakaa saa moja, naweza nikakaa mwaka mmoja. Kwa hiyo kama mtendaji hamtaniona kwenye majukwaa kwa sababu wapo waliopewa dhamana ya kukaa kwenye majukwaa.”

Alisema kazi yake ni kubuni mikakati ya kutekeleza, kutoa taarifa kwenye vikao na kusimamia maelekezo ya chama.

Alisema mambo matatu atakayotekeleza katika sekretarieti ni bidii ya kazi, maarifa ya kutenda kazi na nidhamu.

-->