Dk Kigwangalla asema ataendelea kuongoza Wizara ya Maliasili

Muktasari:

  • Dk Kigwangalla amesema hahongeki na kama ni umasikini ni bora kufa njaa.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Hamisi Kigwangalla amesema ataendelea kuwepo ndani ya wizara hiyo kama kilichowafanya watangulizi wake kuondoka ni masilahi binafsi, kwa kuwa hahongeki, hashawishiki na aliyemteua analifahamu hilo.

 “Sitakuwa tayari kupoteza heshima yangu, aliyeniteua anajua kuwa mimi ni muarobaini wa hayo yote, hata nilipoteuliwa walianza kunidhihaki kupitia mitandao ya kijamii kuwa ninakwenda kuharibikiwa huko, eti kwa sababu mawaziri hawadumu, haipo hiyo,” amesema Dk Kigwangalla leo Jumapili Oktoba 22,2017 mjini Dodoma.

Amesema hayo akijibu kauli ya Meya wa Jiji la Arusha, Kalist Lazaro aliyemtahadharisha kuwa mawaziri wamekuwa hawadumu ndani ya wizara hiyo kutokana na kununulika na wadau kwa kuwa kuna ushawishi mwingi.

Hayo yameibuka kwenye mkutano wa wadau wa sekta mbalimbali zinazofanya kazi na Wizara ya Maliasili na Utalii ambao Dk Kigwangalla alikutana nao akiwa na Naibu Waziri wake, Japhet Hasunga.

Katika mchango wake, Meya Lazaro amesema, “Niliwahi kumtahadharisha waziri mwenzako Hamisi Kagasheki kuwa hatadumu katika wizara hiyo kutokana na wadau kuwa na vishawishi vingi, leo hii naomba kukuambia kuwa sheria hizo mnazosema kuwa ni mbovu si kweli bali zinakosa usimamizi wa kutosha kwa sababu ya masilahi ya watu.”

Meya Lazaro amemtaka waziri kukutana na kila sekta ili kusikiliza kilio chao akisema ndani ya wizara hiyo kama atapatikana mtu wa kuisimamia vizuri inaweza kutoa mchango mkubwa ambao haujapata kutokea lakini akaahidi kuwa watamsaidia ili adumu kuliko mawaziri wengine.

Amesema “Napenda uendelee kubaki katika wizara hii, wewe ni kijana mdogo nisingependa uwe geti la kutokea.”

Mawaziri waliowahi kuiongoza wizara hiyo ni Anthony Diallo (2005-2006), Profesa Jumanne Maghembe (2007-2008; 2016-2017), Shamsa Mwangunga (2008-2010), Ezekiel Maige (2010-2012), Balozi Hamis Kagasheki (2012-2013) na Lazaro Nyalandu (2014-2015).

Meya Lazaro amesema baadhi ya mawaziri wamekuwa wakiitwa na makundi mbalimbali akitoa mfano wa wawindaji na kuzungumza nao lakini hushawishika kuegemea huko na wakiitwa na watu wengine huegemea huko, hivyo kushindwa kubaki katikati ya sekta zote.

Akijibu hoja hiyo, Dk Kigwangalla amesema hana shaka ya aina yoyote kuhusu kupewa wizara hiyo.

Dk Kigwangalla amewatahadharisha wadau akisema wanapofika ofisini kwake wajiandae vyema, vinginevyo anaweza kusimama na kumuacha mtu kama atagusa suala la rushwa.

“Mimi sihongeki, kwa hivyo siko tayari kung’oka kwa sababu yoyote ile, kama ni umasikini ni bora kufa njaa, kwangu fedha haiwezi kunitolea heshima licha ya kuwa wote tunazitaka,’’ amesema.

Waziri huyo amejisifu kuwa hata aliyemteua anajua yeye ni muarobaini, hivyo imani yake ni kubwa kwake na kwa upande wake hatakuwa tayari kuona akiharibikiwa njiani.