Dk Kigwangalla awashukia viongozi hospitali Bukombe

Naibu Waziri wa Afya, Dk Hamisi Kigwangalla (mwenye shati la drafti)

Muktasari:

Dk Kigwangalla alitoa agizo hilo juzi alipotembelea hospitali hiyo kukagua mazingira ya utoaji huduma.

Bukombe. Naibu Waziri wa Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Hamisi Kigwangalla ametoa siku 90 kwa Hospitali ya Wilaya ya Bukombe kutengeneza mashine za kuchanganya dawa ya usingizi zilizoharibika miezi sita iliyopita.

Dk Kigwangalla alitoa agizo hilo juzi alipotembelea hospitali hiyo kukagua mazingira ya utoaji huduma.

Naibu waziri huyo alishtushwa na viongozi wazembe waliotelekeza vifaa hivyo na kuviweka stoo.

“Hamna uchungu na vifaa hivyo, kwasababu hamjui gharama yake, kimoja kinanunuliwa Sh120 milioni, kwa maana hiyo mnafanya kazi kwa mazowea ili muwatese wananchi wenye hali ya chini wanaofika kupata huduma hiyo,” alisema Dk Kigwangalla.

Alimtaka  Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo kushirikiana na Mganga Mkuu kufanya marekebisho kwenye chumba cha upasuaji kama inavyotakiwa kitaalamu.