Dk Kijaji aiponda hotuba ya upinzani bungeni

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dk Ashatu Kijaji akizungumza bungeni wakati akijibu hoja za wabunge kuhusu mapendekezo ya Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa mwaka wa Fedha 2019/20 jijini Dodoma leo, ambapo amesema hotuba ya kambi ya upinzani iliyosomwa bungeni ina lengo la kuipotosha serikali. Picha na Ericky Boniphace

Muktasari:

  • Naibu Waziri Dk Kijaji amesema hotuba ya upinzani bungeni iliyowasilishwa na Halima Mdee kuhusu Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka wa fedha 2019/2020 ilinukuliwa kutoka kwa mhuni

Dodoma. Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji ameikosoa na kuipinga hotuba ya kambi ya upinzani bungeni akisema ilinukuliwa kwa mhuni.

Akichangia katika hotuba ya mpango wa Serikali katika kuhitimisha hoja hiyo leo Jumatatu Novemba 12, 2018, Dk Kijaji amesema hotuba hiyo imejaa upotoshaji mkubwa.

Novemba 6, 2018 msemaji wa kambi ya upinzani bungeni, Halima Mdee aliwasilisha maoni ya kambi hiyo ikionyesha asilimia 47 ya Watanzania ni maskini.

"Huyu atuambie alipata wapi hizi takwimu, tumeona amenukuu kwa mhuni, nami namuita mhuni kwa sababu hajaeleza aliwahoji wapi Watanzania na ni wangapi, lakini mheshimiwa Mdee naye ni mwanasheria bali aliibeba kama ilivyo," amesema Dk Kijaji.

Naibu waziri huyo amesema kila kitu kipo sawa ikiwemo hoja ya kuwa ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) ambao amesema mradi huo unajengwa kwa fedha za ndani lakini hauzuii anayetaka kuwekeza au kusaidia.

Kwa mujibu wa Dk Kijaji, Sh6.5 trilioni zimetumika katika utekelezaji wa mpango kwa kipindi cha 2016/17 lakini mradi wa reli pekee umegharimu  Sh1.22 trilioni.

Wakati huohuo, Dk Kijaji amewaomba wachumi nchini kuanzisha chama chao ili wawe wasemaji na watoe ushauri kuhusu masuala ya uchumi.