Dk Kimei: Rais Magufuli alipendekeza CRDB kuwa na tawi Chato

Muktasari:

 Hayo yameelezwa leo na Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB, Charles Kimei

Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB, Dk Charles Kimei amesema kuanzishwa kwa tawi la benki hiyo wilaya ya Chato ni kutokana na utafiti uliofanywa na  Rais John Magufuli.

Akizungumza leo Ijumaa Machi 9, 2018 wilayani humo katika ufunguzi wa tawi la benki hiyo, Dk Kimei amesema Magufuli akiwa waziri aliomba kufunguliwa kwa tawi la benki hiyo Chato.

Kimei amesema alimweleza Magufuli kuwa isingekuwa rahisi kwa sababu hakuna biashara katika wilaya ya Chato.

"Akanieleza kwamba no research no right to speak (kama hujafanya utafiti huna haki ya kuzungumza)," amesema.

Kimei amesema baada ya kauli hiyo alituma watumishi kwenda Chato ili kufanya utafiti kama wanaweza kufungua tawi, kwamba vijana waliporudi walimweleza kwamba Chato hakuna biashara ya kuwafanya wafungue benki.

"Nilimweleza Magufuli kuhusu utafiti ule akaniambia vijana wako wamekosea nitafanya wa kwangu na nitakuletea," amesema.

Kimei amesema baada ya muda Magufuli alimpelekea utafiti na walipouona wakaamua kuanzisha tawi la benki hiyo Chato.

Amemshukuru Rais kwa mchango mkubwa uliowezesha kufunguliwa kwa tawi hilo.

Amependekeza benki hiyo kuitwa JPM tawi CRDB Chato.