Dk Kolimba: Kuondolewa kwenye uwaziri ni kama mbio za vijiti

Muktasari:

Aliyekuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje, Dk Suzan Kolimba amemkabidhi ofisi naibu waziri mpya wa wizara hiyo, Dk Damas Ndumbaro


Dodoma.  Aliyekuwa Naibu Waziri  wa Mambo ya Nje, Dk Suzan Kolimba amefananisha  kuenguliwa katika nafasi hiyo na mbio za kijiti, kubainisha kuwa sasa amempabidi kijiti naibu waziri mpya wa wizara hiyo, Dk Damas Ndumbaro.

Akizungumza leo Ijumaa Oktoba 19, 2018 katika makabidhiano ya ofisi, Dk Kolimba amemshauri naibu waziri huyo mpya kuchukua mambo mazuri yaliyofanyika katika kipindi cha miaka mitatu alichokuwa katika wizara hiyo na kuzipatia ufumbuzi changamoto alizoziacha.

“Anao wasaidizi ambao ni wakurugenzi waliopo katika vitengo mbalimbali lakini kuna ofisi ya katibu mkuu na waziri mwenye dhamana wakishirikiana kwa pamoja  na wakiendana na misingi iliyoweka Mungu atawasaidia na wataweza kufanikiwa,” amesema Dk Kolimba.

Amesema matarajio yake yanafanana na yale ambayo Rais aliyasema wakati anamwapisha Dk Ndumbaro, kumtaka ajaribu kuangalia kasi ya utekelezaji wa mambo katika wizara hiyo.

“Kwa muda wa miaka mitatu ambayo nimekaa wizara hii naona kwamba Rais amenipendelea lakini pia alinipa heshima kubwa sisemi kwamba wizara nyingine sio nyeti lakini wizara hii ni mahususi na maalumu na ni nyeti kwa masilahi mapana ya nchi,” amesema Dk Kolimba.

“Namshukuru kwa kunipa nafasi hii nyeti ya kutumikia, niseme mimi ni Mtanzania, mzalendo ninaahidi kuwa mwaminifu kama nilivyoapa wakati ule kuwa uaminifu,  uzalendo na uchapakazi  ndiyo utakuwa msingi wake (Dk Ndumbaro) katika utekelezaji wa kazi zake.”