Dk Kolimba: Nimepokea kwa furaha uamuzi wa Rais Magufuli

Muktasari:

Leo Septemba 26,2018, Rais John Magufuli ametangaza mabadiliko madogo ya Baraza la Mawaziri, kwa kumteua Dk Damas Ndumbaro kuwa naibu waziri Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki kuchukua nafasi ya Dk Susan Kolimba

Dar es Salaam. Aliyekuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Susan Kolimba amesema hana kinyongo na Rais John Magufuli kutokana na kumwondoa kwenye wadhifa huo.

Dk Kolimba amesema amepokea kwa furaha uamuzi wake.

Akizungumza na MCL Digital muda mfupi baada ya kupokea taarifa ya kutenguliwa kwake, leo Septemba 26, 2018, Dk Kolimba amesema uongozi ni sawa na mbio za kupokezana kijiti hivyo inakupasa kuwa tayari kukabidhi majukumu kwa mwingine kama inavyoamuliwa na mamlaka ya uteuzi.

“Kile unachotakiwa kufanya ukiwa kwenye wadhifa ni kuchapa kazi kwa nguvu zako zote na kuwa tayari kukabidhi madaraka kwa mwingine pindi mamlaka ya uteuzi inapoamua kufanya hivyo,” amesema Dk Kolimba ambaye ni mbunge wa viti maalum (CCM)

Amesema ataendelea kuwatumikia Watanzania katika maeneo ya kuimarisha maendeleo ya kiuchumi na ustawi wa kijamii kwa vile bado ni kiongozi.

Alipoulizwa sababu za kuondolewa kwenye wadhifa wake huo, Dk Kolimba amesema hawezi kueleza chochote bali mamlaka ya uteuzi ndiyo inayojua.

Dk Susan Kolimba alizaliwa Desemba 8, 1964.  Alihitimu elimu ya sekondari mwaka 1982 katika Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Kibosho na baadaye alijiunga na Chuo cha Ualimu Marangu alikohitimu stashahada yake mwaka 1988 na kuanza kufundisha katika shule za sekondari kwa miaka mitatu.

Alisoma shahada za sheria katika Chuo Kikuu cha Peoples' Friendship cha Urusi. Kabla ya kujitupa kwenye siasa alikuwa mhadhiri katika Chuo Kikuu Huria (OUT).