Dk Magufuli kuuzima Mwenge Bariadi

Muktasari:

Mbali na Rais Magufuli katika kilele hicho, Mke wa Baba wa Taifa Mwl Julius Kambarage Nyerere, Mama Maria Nyerere anatarajia kuhudhuria misa ya maadhimisho ya kumbukumbu ya miaka 17 ya kifo cha mwasisi huyo wa Taifa zitakayofanyikia Kanisa la Mtakatifu Yohana mjini Bariadi. 

Bariadi. Rais John Magufuli anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika sherehe za kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa zitakayozofanyika Bariadi mkoani Simiyu, huku zikitanguliwa na maonyesho ya wiki ya vijana.

Mbali na Rais Magufuli katika kilele hicho, Mke wa Baba wa Taifa Mwl Julius Kambarage Nyerere, Mama Maria Nyerere anatarajia kuhudhuria misa ya maadhimisho ya kumbukumbu ya miaka 17 ya kifo cha mwasisi huyo wa Taifa zitakayofanyikia Kanisa la Mtakatifu Yohana mjini Bariadi.

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Antony Mtaka amesema maadhimisho ya wiki ya vijana yatafunguliwa rasmi Oktoba 8 hadi 14, mwaka huu na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu, Jenisita Mhagama katika uwanja wa Sabasaba mjini humo

“Maadhimisho hayo yataenda sambamba na kongamano la vijana. Katika kongamono hilo kutajadiliwa mada mbalimbali zinazoihusu jamii, ikiwemo kupinga mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi” amesema Mtaka

Kadhalika, Mtaka amesema katika wiki ya vijana kutakuwapo na uchangiaji wa damu kwa hiari kwa ajili ya kuwasaidia watu wenye uhitaji.

Pia amewataka wananchi kuchangamkia fursa hasa katika nyanja za kiuchumi na kijamii kutokana na ugeni mkubwa ambao utaongeza kipato mkoani humo, huku akiwataka kuonyesha ukarimu na ushirikiano pamoja na kuimarisha usafi katika maeneo ya wazi na biashara.