Dk Mashinji, wenzake waendelea kushikiliwa Chadema ikitoa tamko

Muktasari:

Makene alisema sekretarieti imemteua Katibu wa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Emmanuel Masonga kukaimu kazi za kanda hiyo wakati huu ambao mwenyekiti na katibu wakiwa kizuizini.

Dar/Songea. Wakati wanasiasa kutoka vyama vya upinzani na wanaharakati wakilaani kushikiliwa kwa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji na viongozi wengine kuwekwa kizuizini kwa saa 48, chama hicho kimetoa tamko kikitaka waachiwe.

Chadema kimesema kuendelea kushikiliwa kwa viongozi hao ni mwendelezo wa matumizi mabaya ya mamlaka za kiserikali.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Chadema, Tumaini Makene alisema sekretarieti ya chama hicho iliazimia kuzitaka mamlaka zilizoagiza kukamatwa na kuwekwa kizuizini Dk Mashinji na viongozi wengine 10, kuwaachilia huru kabla ya kuchukua hatua nyingine zinazotakiwa ili kulinda uhuru na haki za kikatiba na kisiasa zilizopo kwa mujibu wa sheria za nchi.

Sekretarieti hiyo pia imeelekeza mawakili wa chama hicho kusimamia kesi kuhakikisha masuala ya kisheria yanafuatwa na haki kutendeka, ikisema wakili Edson Mbogoro ndiye atakayesimamia suala hilo.

Makene alisema sekretarieti imemteua Katibu wa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Emmanuel Masonga kukaimu kazi za kanda hiyo wakati huu ambao mwenyekiti na katibu wakiwa kizuizini.

Pamoja na Dk Mashinji, viongozi wengine walioko kizuizini Mbambabay wilayani Nyasa tangu juzi walipokamatwa ni mwenyekiti wa kanda hiyo na Mbunge wa Ndanda, Cecil Mwambe; Philbert Ngatunga ambaye ni katibu wa kanda hiyo na Manawa Samuda, ambaye ni ofisa wa operesheni na mafunzo.

Wengine ni mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Ruvuma, Zubeda Sakuru; Asia Mohamed (ofisa wa kanda), Ireneus Ngwatura (mwenyekiti wa Mkoa wa Ruvuma), Delphin Ngaiza (katibu wa Mkoa wa Ruvuma) Cuthbert Ngwata (mwenyekiti Wilaya ya Nyasa) na Charles Makunguru (katibu wa uenezi Wilaya ya Nyasa).

Wakati Chadema ikitoa tamko hilo, Mkuu wa Wilaya ya Nyasa, Isabela Chilumba alisema utaratibu wa kuwafikisha mahakamani viongozi hao unafanyika. “Tunawashikilia viongozi mbalimbali  wa Chadema kwa agizo la mkuu wa mkoa,  tayari wameanza kuhojiwa. Utaratibu wa kisheria unakamilishwa watafikishwa mahakamani,” alisema Chilumba.

Wakili Mbogoro alisema ameshawasiliana na viongozi wa Chadema na ameagizwa kufuatilia kesi hiyo.

“Kwa kuwa leo (jana) si siku ya kazi na saa 48 alizotoa mkuu wa mkoa zinaisha kesho (leo), ninafanya utaratibu waweze kuachiwa baada ya kufikishwa mahakamani na bahati mbaya viongozi wetu karibu wote wa mkoa wapo ndani,” alisema Mbogoro.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Gemini Mushy alisema wanaendelea kuwashikilia viongozi hao na kuwataka viongozi, wananchi na wanachama wa vyama mbalimbali kufuata sheria na maelekezo yanayotolewa na Serikali.

Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Zanzibar), Salum Mwalimu alisema misukosuko wanayopata viongozi wa chama hicho ikiwa ni pamoja na kukamatwa na Jeshi la Polisi imewaimarisha zaidi badala ya kuwanyong’onyeza.

“Sisi hatuyumbishwi, bali tunaimarishwa. Kukamatwa, kunyanyaswa au kufungiwa biashara zetu ni kutuimarisha, ndiyo maana leo unaisikia Chadema na CUF tu,” alisema Mwalimu.

Mkurugenzi wa Habari na Uhusiano wa Umma wa CUF, Salim Bimani amelaani kushikiliwa kwa viongozi hao.

“Viongozi wa upinzani kukamatwa bila sababu za msingi ni ukandamizaji kwa wapinzani na suala hilo halijengi nchi, bali linachochea chuki kati ya watu ambao wengi wao ni walipakodi kama ilivyo kwa wananchi wengine,” alisema Bimani.

Bimani alisema wanashangaa kuona katika vikao vya ndani vya Chama cha Mapinduzi (CCM) hakuna kiongozi anayekamatwa.

Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), kwa upande wake, umewataka wakuu wa mikoa na wilaya kutotumia vibaya mamlaka yao kwa kuwakamata wananchi ovyo na kuwaweka rumande.

Mratibu wa Taifa wa mtandao huo, Onesmo Olengurumwa alisema  Sheria ya Tawala za Mikoa ya Mwaka 1997 inatakiwa kurekebishwa ili kuondoa vifungu vinavyowapa nguvu kubwa inayowakandamiza wananchi.

Alisema kumekuwa na maagizo mengi ya wakuu wa wilaya ya kuwakamata wananchi bila ya kuwa na sababu za msingi.

Alisema tangu kuanza kwa mwaka huu hadi sasa, kuna matukio zaidi ya 20 ambayo yanaminya haki za binadamu yakiwamo ya kuminya haki ya kufanya siasa kinyume na Katiba.

“Ukiwa mwanasiasa una haki za msingi za kufanya mikutano kama njia ya kuwasiliana na wananchi lakini haki hii tumeshuhudia inaminywa, mbaya zaidi sasa hata mikutano ya ndani inazuiwa,” alisema.

Imeandikwa na Joyce Joliga, Elias Msuya, Prosper Kaijage na Raymond Kaminyoge.