Dk Mpango abanwa uhaba wa ajira kwa vijana

Mbunge wa Viti Maalum (CUF), Kiza Mayeye akizungumza bungeni alipokuwa akichangia mjadala wa kupitisha Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2018/2019, jijini Dodoma leo. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

  • Wabunge wa CUF na Chadema wamtaka aeleze mkakati wa Serikali kumaliza uhaba huo wa ajira

Dodoma. Wabunge wa Viti Maalumu, Mariam Msabaha (Chadema) na Kiza Mayeye (CUF) wamemtaka Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango kuelezea mkakati madhubuti wa kutatua uhaba wa ajira kwa vijana.

Wametoa kauli hiyo leo Ijumaa Juni 22, 2018 bungeni mjini Dodoma wakati wa mjadala wa bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha wa 2018/19.

Mayeye amesema tatizo la ajira nchini linawafanya vijana kujiingiza katika matukio hatarishi kwa ajili ya kujitafutia riziki na kumtaka waziri huyo wakati akijibu hoja za wabunge zilizoibuliwa katika mjadala huo, kueleza mkakati wa kuwakwamua vijana.

“Mnasema vijana wajiajiri, hivi kijana anawezaje kujiajiri wakati mtaji hana. Kama mnasema kujiajiri wekeni mipango na mikakati ili vijana wajiajiri, wapeni mitaji,” amesema.

“Waziri Mpango katika kitabu chako cha bajeti hujaelezea ajira kwa vijana ni mkakati upi na sisi tupo katika hatari gani ya tatizo hili jambo linalowafanya vijana kukimbilia nje ya nchi kutafuta ajira.”

Amesisitiza kuwa, “wekeni mkakati wa kusaidia upatikanaji wa ajira ili kuwawezesha vijana kupata kipato, hususan akinadada ambao wanajiingiza katika njia zisizo stahili kujipatia fedha.”

Kwa upande wake, Msabaha amehoji,“hizi ajira mpya ambazo mnasema zinatoka, zitatoka lini? Na hawa wanaokaimu watakaimu hadi lini na ajira hizo za Muungano zitakuwa ngapi? Tunataka kujua hizo ajira.”