Dk Mpango akagua EFD duka kwa duka Dodoma

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango   

Muktasari:

Dk Mpango pia alishangazwa na kitendo cha mashine 100 za EFD kuharibika kwa siku mbili akisema kwamba jambo hilo kwake haliingii akilini.

Dodoma. Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango, amefanya ziara ya kushitukiza katika mitaa ya mji wa Dodoma na kubaini baadhi ya wafanyabiashara hawatumii ipasavyo mashine za kieletroniki za kukusanyia kodi ya Serikali-EFDs.

Baada ya kubaini hilo Dk Mpango akawaonya wafanyabiashara kote nchini kuacha mchezo huo.

Dk Mpango aliyeambatana na baadhi ya maofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoa wa Dodoma, amebaini baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu hawatoi risiti huku wengine wakiandika kiwango kidogo cha fedha kwenye risiti hizo.

Mmoja wa wafanyabiashara aliyekumbana na mkono wa Waziri Mpango, ni Isdori Shirima ambaye amekiri kufanya makosa ya kutotumia mashine hizo ipasavyo

“Naomba unisamehe mheshimiwa, sitarudia tena unajua sisi vijana tunabangaiza, lakini nimebaini nimefanya makosa” amesema.

Hata hivyo Dk  Mpango ameiagiza TRA Dodoma, kufanya ukaguzi wa kina wa mahesabu ya mfanyabiashara huyo ili kubaini kiwango cha kodi alichokwepa na kumchukulia hatua stahiki.

Pia ameiagiza TRA Dodoma kuwapeleka ofisini kwake mawakala wote mkoani humo wanaosambaza mashine za kieletroniki za kukusanyia mapato EFDs baada ya kubaini kuwa zaidi ya mashine 100 zimeharibika na hazitumiki tangu jana.

“Kuna kitu sikielewi na hakiingii akilini, inakuwaje mashine ziharibike kwa kiwango hicho, mashine 100 kuharibika kwa siku mbili ni nyingi na ina maana nimekosa mapato mengi,” alisema

Aliagiza mawakala wote wanaosambaza ama kuuza mashine hizo wakutane naye ofisini kwake mjini humo ili kubaini tatizo na kuongeza kuwa haiwezekani wafanyabishara walipie mashine hizo zaidi ya mwezi uliopita lakini hawapelekewi hali inayozidi kuikosesha Serikali mapato yake.

Baadhi ya wananchi na wafanyabiashara wamepongeza uamuzi wa Serikali wa kulivalia njuga suala la kodi na kwamba wako tayari kuiunga mkono Serikali kwa kutoa risiti wanapouza bidhaa na kudai risiti zenye viwango sahihi vya manunuzi waliyoyafanya ili kuijengea Serikali uwezo wa kuihudumia jamii.

Dk Mpango ametembelea pia baadhi ya vituo vya mafuta mjini humo na kuwakumbusha wamiliki wote wa vituo vya mafuta kuzingatia agizo la Serikali linalowataka wafunge mashine maalumu za kielektroniki zinazofungwa kwenye pampu za mafuta ndani ya siku 14 ambazo ziko ukingoni.