Dk Mpango asema kuomba misaada ni aibu kwa Taifa

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango

Muktasari:

Dk Mpango amesema ni lazima kufanya kazi ili kuondokana na kuomba kwa mataifa ya nje.

Dodoma. Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango amesema amechoka kuomba misaada nchi za nje kwa sababu ni aibu na hilo linalidhalilisha Taifa.

Dk Mpango amesema hayo leo Jumamosi Novemba 18,2017 alipofunga mafunzo ya wadadisi, wasimamizi na wahariri wa takwimu za mapato na matumizi binafsi katika ngazi ya kaya.

"Lazima tufanye kazi kwelikweli. Mimi kwa miaka kadhaa natumwa kwenda kutafuta misaada huko nje ya nchi, nimechoka. Imekuwa ikidhalilisha Taifa, wanasema kweli sisi ni nchi ya tatu katika upatikanaji wa dhahabu halafu waziri wao wa fedha  anakuja kuomba," amesema.

Dk Mpango amesema ni lazima kama nchi iwe na mkakati kuondokana na hali hiyo na kwamba, malengo yatafikiwa kama makusanyo ya takwimu yatafanyika na kutumiwa kwa weledi na umakini.

"Hamna budi kufuata sheria na kanuni za utumishi. Taarifa mtakazozipata ni za siri hamtakiwi kutoa kokote ni kwa ajili ya matumizi ya takwimu pekee. Mkifanya vinginevyo Mahakamani," amesema.

Dk Mpango amesema watakaovuruga kazi  inayoanza mwezi huu na kumalizika baada ya miezi sita watabanwa.

"Siku za nyuma kuna watu walikwenda kukusanya takwimu wakaleta tukaanza kuulizana ni kwa nini idadi ya watu imepungua? Kumbe walikwenda kupika takwimu katika mikorosho, msiende kutusaliti," amesema.

Amezitaka kaya zilizochaguliwa kutoa taarifa sahihi wanapofikiwa na wadadisi wa takwimu na viongozi wa ngazi ya Taifa hadi vijiji kutoa ushirikiano kwa wadadisi wanapofika kwenye maeneo yao.

Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Takwimu, Dk Albina Chuwa amesema kwa kutumia teknolojia wameweza kupunguza matumizi kutoka Sh20 bilioni hadi Sh10 bilioni, fedha ambazo zitakamilisha kazi hiyo.

Amesema huo ni utafiti wa saba na kwamba, watahakikisha wanatoa matokeo ya awali ya utafiti katika kipindi cha miezi sita kuanzia sasa ili yaweze kufanyiwa kazi.

"Nendeni mkafanye kazi kwa uadilifu na uaminifu mkubwa bila kufanya udanganyifu wowote maana hatutashindwa kuchukua hatua kwa wale wote watakaobainika kufanya udanganyifu," amesema.

Dk Chuwa amesema kaya zisizopungua 10,460 zitahusika katika utafiti huo utakaohusisha wadadisi 620 baada ya wengine kuondolewa baada ya kushindwa mtihani kwa kupata chini ya asilimia 60.