Dk Nchemba ataka wanasiasa kuwa na subira

Muktasari:

  • Mwaka 2019 kutafanyika uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu mwaka 2020

Moshi. Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba amewataka wanaolalamikia kuzuiwa mikutano ya siasa watoe mifano ya nchi ambazo demokrasia imekua kwa kuruhusu mikutano hiyo.

Dk Nchemba amesema hayo leo Juni 17, 2018 kwenye mahafali ya kwanza ya vijana wa CCM wa vyuo vikuu Mkoa wa Kilimanjaro.

Amesema kumekuwapo malalamiko ya kuminywa demokrasia jambo ambalo si sahihi.

Dk Nchemba amesema wanaosema demokrasia imeminywa, wanapandikiza chuki.

"Tupeni nchi zinazofanya mikutano ya hadhara kujenga vyama baada ya uchaguzi mkuu kwa kuwa hata nchi za mfumo wa vyama vingi hazifanyi hivyo," amesema Dk Nchemba.

Amesema wananchi wanapaswa kutambua sasa ni muda wa kazi na wa mikutano utafika watakaporuhusiwa kuingia uwanjani kunadi sera zao.

Dk Nchemba amesema mwaka 2019 ni wa uchaguzi wa serikali za mitaa na 2020 ni uchaguzi mkuu, hivyo vyama vyote vitaruhusiwa kuingia uwanjani kunadi sera.