Dk Nchimbi amweka ‘kikaangoni’ Mwakibinga

Dk Emmanuel Nchimbi

Muktasari:

Pamoja na hilo, Dk Nchimbi kupitia Kampuni ya Uwakili ya FK Law Chambers, pia amemtaka Mwakibinga kumlipa Sh2.5 bilioni kwa madai kuwa maneno aliyoyatoa yamemchafua, kumdhalilisha na kumuonyesha kama mtu asiyefaa kuwa kiongozi, mtu hatari, mwizi na mbadhirifu.

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini la Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Dk Emmanuel Nchimbi ametoa siku 14 kwa kada wa chama hicho, James Mwakibinga kumuomba radhi kupitia vyombo vya habari vinginevyo atamfikisha mahakamani.

Pamoja na hilo, Dk Nchimbi kupitia Kampuni ya Uwakili ya FK Law Chambers, pia amemtaka Mwakibinga kumlipa Sh2.5 bilioni kwa madai kuwa maneno aliyoyatoa yamemchafua, kumdhalilisha na kumuonyesha kama mtu asiyefaa kuwa kiongozi, mtu hatari, mwizi na mbadhirifu.

Mwakibinga alifanya mkutano na waandishi wa habari Agosti 16, mwaka huu na kumtuhumu Dk Nchimbi kuhusika katika uuzwaji kinyemela wa viwanja 200 vya UVCCM Temeke na kuwa mpaka sasa vimebaki viwanja vinne.

Kada huyo wa CCM alisema, Dk Nchimbi anatajwa kupewa sehemu katika jengo jipya la UVCCM lililopo makutano ya Barabara za Lumumba na Morogoro jijini Dar es Salaam.