Dk Shein aongoza Kamati Maalumu kupiga panga wagombea uwakilishi

Makamu mwenyekiti wa CCM, Zanzibar ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein akiongoza Kikao cha Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Zanzibar,  kilichofanyika mjini Zanibar juzi.Picha na CCM ZANZIBAR

Muktasari:

  • CCM yawataka wanachama wake kujiandaa kupiga kura huku ikijihakikishia ushindi

Unguja. Makamu mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein ameongoza kikao cha Kamati Maalumu ya Halmashauri Kuu ya Taifa Zanzibar cha kujadili majina ya wanachama walioomba nafasi ya uwakilishi wa Jimbo la Jang’ombe.

Wanachama walioomba ni Lilian Grace Lyimo, Othman Shaaban Kibwana na Ramadhan Hamza Chande.

Naibu katibu mkuu wa CCM Zanzibar, Dk Abdallah Juma Sadalla maarufu Mabodi alisema majina ya wanachama hao sasa yatapelekwa kwa ajili ya kujadiliwa katika kikao cha Kamati Kuu.

Alisema kikao hicho kitateua jina la mgombea mmoja ambaye atapeperusha bendera ya CCM katika uchaguzi mdogo wa jimbo hilo utakaofanyika Oktoba.

Dk Mabodi alisema licha ya wanachama hao kupigiwa kura awali na kuwapo mshindi wa kwanza hadi wa tatu, Kamati Kuu inaweza kumpitisha hata aliyeshika nafasi ya tatu ikiona wengine hawana sifa zaidi yake.

Aliwataka wanachama hao kujiweka tayari kupiga kura huku akitamba mgombea wao atashinda kutokana na mipango mizuri waliyojiwekea.

Pia, Dk Mabodi alisema wajumbe walijadili utaratibu wa kampeni utakavyokuwa kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (Zec).

Alisema CCM imejipanga kuendelea kuongoza jimbo hilo kutokana na kukubalika kwake.

Uchaguzi mdogo huo unafanyika kufuatia hatua ya chama hicho kumvua uanachama aliyekuwa mwakilishi wake, Abdallah Diwani.

Katika hatua nyingine, kamati hiyo imetuma salamu za rambirambi kwa mwenyekiti wa CCM, Rais John Magufuli kutokana na kupinduka kwa kivuko cha Mv Nyerere.

Dk Mabodi alisema wanachama wa CCM wamepokea kwa masikitiko taarifa ya maafa hayo hivyo wanaungana na Watanzania wote katika kuomboleza msiba huo.

“CCM tunaeleza umma kwamba msiba huu umetugusa Watanzania wote kwani waliopata ajali ni ndugu na jamaa zetu, hivyo tunawaomba wananchi tuungane na kuweka kando tofauti zetu ili tuomboleze kama taifa,” alisema.

Naye Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi akizungumzia msiba huo alisema ni mkubwa ambao umegusa kila moyo wa mwananchi.

Balozi Iddi alisema kwamba kutokana na msiba huo Serikali imefuta sherehe ya Elimu Bila Malipo kwa mwaka huu iliyokuwa ifanyike Septemba 23. Alisema lengo ni kuonyesha umoja, upendo, undugu na urafiki.