Dk Tizeba apokewa na kilio cha madhara ya tembo, vifo

Muktasari:

Licha ya waziri huyo kulenga zaidi uhamasishaji wa zao la pamba, wakazi wa Kitongoji cha Nyakitono vijiji vya Makundusi na Natta waliwasilisha kilio hicho wakiomba Serikali kuchukua hatua stahiki ili kuwanusuru na madhara hayo ikiwemo vifo na majeruhi kwa watu.

Kilio cha madhara ya tembo kuharibu mazao pamoja na vifo kwa wakazi wa Wilaya ya Serengeti mkoani Mara kimetawala ziara ya Waziri wa Kilimo, Dk Charles Tizeba.

Licha ya waziri huyo kulenga zaidi uhamasishaji wa zao la pamba, wakazi wa Kitongoji cha Nyakitono vijiji vya Makundusi na Natta waliwasilisha kilio hicho wakiomba Serikali kuchukua hatua stahiki ili kuwanusuru na madhara hayo ikiwemo vifo na majeruhi kwa watu.

Kwa mujibu wa taarifa ya wilaya, uharibifu wa mazao ya vyakula, vifo vya watu na mifugo tangu mwaka 2009 hadi 2016 huku ekari 7557.86 za mazao yenye thamani ya zaidi ya Sh1 bilioni ziliharibiwa. Pia, mifugo 409 yenye thamani ya Sh53.6 milioni iliuawa na wanyamapori huku katika kipindi cha 2015 na 2016 watu wanne waliuawa na tembo.

Mkazi wa kijiji hicho, James Makuru alisema tatizo la tembo ni kubwa na linachangia upungufu wa vyakula na umaskini.

“Tunaomba Serikali ichukue hatua za makusudi kudhibiti, mnahimiza kilimo wakati tembo wanamaliza vyakula,” alisema.

Alisema pamoja na mikakati mbalimbali ya kudhibiti tembo ikiwemo waya, pilipili, mafuta, kupiga madebe na ulinzi wa usiku hawajafanikiwa na hali inazidi kuwa mbaya kila uchwao huku wananchi wengi wakikata tamaa.

Mkazi wa Kijiji cha Natta, Mangarai Nyamasagi alisema hata kifuta machozi hawapati kama ilivyobainishwa kwenye Sheria ya Wanyamapori namba 5 ya mwaka 2009 kuhusu ulipaji fidia.

Hata hivyo Dk Tizeba aliwataka kutolima maeneo ambayo ni mapito ya wanyama kwa kuwa kuendelea kufanya hivyo ni kuwakaribisha wanyama hao ambao kihistoria wana kumbukumbu ya maeneo waliyowahi kupita. “Dawa rahisi ya kufukuza tembo ni kuchoma pilipili nyingi wakati upepo unaelekea walipo, hawawezi kurudi tena maana harufu yake inawaumiza. Pia imarisheni doria za askari ili kudhibiti tatizo,” alisema.

Mkuu wa wilaya hiyo, Nurdin Babu alisema halmashauri imenunua gari la pili la doria za mara kwa mara.