Dk Tulia awataka wabunge wa viti maalumu wasiwatelekeze wananchi

Muktasari:

35 milioni: Kiasi cha fedha kilichokusanywa katika harambee.

320,000: Kiasi ambacho kila kikundi kilichokusudiwa mkoani Songwe kitapata

Mbozi.  Naibu Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson amewataka wabunge wa viti maalumu kutekeleza kwa vitendo ahadi walizozitoa kwa wananchi wakati wakipigiwa kura badala ya kuwatelekeza kwa kisingizio cha kutokuwa na majimbo.

Akiendesha harambee ya kuendeleza mfuko wa uwezeshaji kiuchumi  wanawake wa CCM wa Mkoa wa Songwe ulioanzishwa na Mbunge wa Viti Maalumu, Juliana Shonza, Dk Tulia alisema wapo wabunge ambao hawatekelezi kwa vitendo yale waliyowaahidi wananchi wao kwenye eneo husika na anapojitokeza mtu mwingine na kutekeleza yaliyoahidiwa wakati wa kampeni mbunge wa eneo husika hukasirika.

“Shonza ahsante sana kwa somo hili na kwa kiasi hiki cha Sh35 milioni, kila kikundi kitapata Sh320,000 badala ya Sh200,000 ulizoahidi.  Hivyo basi niwaombe sana wabunge hasa wa CCM kuiga mfano mzuri wa hiki tunachoshuhudia leo hii kutoka kwa Mbunge Shonza kwa kutekeleza ahadi alizozitoa kwa wananchi wakati wa kupigiwa kura lakini pia kwa kutekeleza ilani ya CCM,” alisema Dk Tulia.

Katika harambee hiyo, Shonza alitoa Sh20 milioni ikiwa ni ahadi ya kukipatia mtaji wa Sh200,000 kila kikundi cha wanawake hao ambao wameanzisha miradi ya ujasiriamali na wadau waliofika kuunga mkono jitihada za mbunge huyo walichangia Sh15 milioni.

Shonza alisema baada ya kupewa ridhaa  kuwa mbunge,  alianza kukutana na wanawake mbalimbali wa mkoa huo kwa ajili ya kuwahamasisha kujiunga katika vikundi vya ujasiriamali na alivisimamia hadi vikapata usajili na kuwapa elimu ya ujasiriamali ili waweze kuanzisha mradi wowote utakaowawezesha kujikopesha wenyewe.