Dodoma ilivyojipanga kudhihirisha kuwa jiji

Muktasari:

Aprili 26, katika hotuba ya dakika 31 aliyoitoa kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma kuadhimisha sherehe za Muungano, Rais John Magufuli aliutangaza mji wa Dodoma kuwa jiji la sita, likitanguliwa na Dar es Salaam, Mwanza, tanga, Mbeya na Arusha.

Dar es Salaam. Ni miaka miaka miwili na nusu sasa tangu Rais John Magufuli alipotangaza kuwa Serikali itahamia Dodoma ili kutimiza ndoto ya miaka mingi kuhamia katika mji huo mkuu wa Tanzania.
Aprili 26, katika hotuba ya dakika 31 aliyoitoa kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma kuadhimisha sherehe za Muungano, Rais John Magufuli aliutangaza mji wa Dodoma kuwa jiji la sita, likitanguliwa na Dar es Salaam, Mwanza, tanga, Mbeaya na Arusha.
Hata hivyo, kuhamia kwa Serikali Dodoma kumelifanya jiji hilo liweze kujipanga ili kukaa katika muonekano mpya.
Kutokana na hali hiyo mipango mbalimbali imewekwa na halmashauri ya jiji katika kuhakikisha Serikali na wafanyakazi wanaohama kutoka jijini Dar es Salaam wanapata huduma zote zinazohitajika kwa wakati.
Dodoma iko umbali wa kilomita 485 kutoka Dar es Salaam, kilometa 264 kutoka Iringa, 441 kutoka Arusha na kilomita 243 Singida
Ni mji mkuu mpya ambao upo katikati ya nchi na ni kitovu cha mtandao wa barabara kuu ukiunganisha Kanda ya Mashariki, Magaharibi, Kaskazini na Kusini.
Mji unavyokuwa kwa kasi, mahitaji ya huduma za burudani na starehe yanaongezeka kama sehemu muhimu ya maisha ya watu.
Akizungumzia mahitaji hayo Mkurugenzi Mtendaji wa Jiji la Dodoma, Godwin Kunambi anasema kwa sasa kuna mahitaji ya maeneo ya burudani, bustani za wanyama na viwanja vya michezo.
“Tunajenga eneo la burudani pale Chinangali kuwe na sweeming pool, table tennis, eneo la watu kupumzikia hivyo mwakani mwezi wa kumi watu watakuwa wanafurahi hapo,” anasema Kunambi.
“Tumegundua weekends (siku za mwisho wa wiki) watu wengi wanakwenda Dar kwa ajili ya burudani, hivyo tunataka wawe wanabaki hapa.”
Anasema jiji limeandaa maeneo kadhaa ya uwekezaji kwa kuwapatia waendelezaji likiwemo eneo la uwekezaji Njedengwa ambalo lina hekta 580 na jumla viwanja 141  vyenye ukubwa wa kati ya eka mbili hadi 26 kwa kiwanja kimoja.
“Mji mpya wa Iyumbu una viwanja 242, kati ya hivyo vya biashara 10, viwanda vidogo viwili, biashara na makazi 173 na makazi maalum 57,” anasema.
Mkurugenzi huyo anasema kama jiji watakuwa na kituo cha biashara ambacho kitazikutanisha taasisi mbalimbali za biashara kama Mamlaka ya Mapato (TRA), (Wakala wa Afya Mahala pa Kazi (Osha) na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) wakiwemo jiji kwa ajili ya leseni za biashara mbalimbali.
“Wadau wote wa biashara wawe pale ili siku moja mtu awe na uwezo wa kupata leseni yake ya biashara,” anasema Kunambi.
Anasema Jiji la Dodoma linajenga kituo kikubwa cha kisasa cha mabasi katika eneo lenye ukubwa wa eka 87. “Stendi ina uwezo wa kuingiza mabasi 250 kati ya hayo waiting (yanayosubiri) ni 150 na ambayo yako on board (yanayohudumia abiria) ni 100,” anasema.
“Sekta binafsi inaweza kushiriki katika ujenzi wa majengo ya biashara kama maduka makubwa ya kisasa.”
Kunambi anasema kutokana na Dodoma kuwa katikati ya Tanzania na ni kitovu cha barabara za kutoka kona zote za ndani na nchi jirani ni kituo muhimu kwa mizigo inayopitishwa kwa njia ya barabara na reli.
“Manispaa inajenga lorry park (maegesho ya malori) ya kisasa eneo la Nala, kwa hiyo sekta binafsi inaweza kushiriki katika ujenzi wa vituo vya malori na majengo ya biashara kama maeneo ya kupakilia na kushushia mizigo, huduma za jamii (zahanati, huduma za mabafu na vyoo).”
Anasema kuna fursa kubwa za kuwekeza katika bandari kavu na maghala makubwa ya kuhifadhia mizigo na jiji lina eneo lenye ukubwa wa hekta 507 kwa ajili ya bandari ya nchi kavu.

Mji wa Serikali
Ukiwa unaingia Dodoma kutokea Dar es Salaam kilomita 17 kutoka katikati utaona kibao cha kuonyesha mji wa Serikali unapojengwa.
Eneo hilo lipo katika Kata ya Mtumba na lina ukubwa wa hekta 617.15 (sawa na eka 1,542.88).
Mji huo kwa upande wa Magharibi utapakana na kambi ya Jeshi ya Ihumwa, Kusini unapakana na barabara iendayo Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa ripoti ya Manispaa ya Dodoma, makadirio ya gharama za kukamilisha mji huo ni Sh10.7 trilioni na zinategemewa kutoka katika vyanzo mbalimbali.
Vyanzo hivyo ni fedha za Serikali, wafadhili, mashirika ya umma, taasisi binafsi na za Serikali pamoja na mashirika binafsi.
“Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma inaendelea kuboresha mandhari ya mji ili kufikia malengo ya kuufanya Mkoa wa Dodoma hasa katika Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma kuwa mji wa kisasa unaoendana na miji ya kimataifa kuwa makao makuu ya nchi,” inaeleza ripoti hiyo ya mwaka huu.

Upakaji rangi
Mpango wa kupaka rangi mapaa ya majengo ni moja ya mikakati katika kuboresha mwonekano wa mji, kuupendezesha na kutofautisha eneo moja na jingine.
Pia, inaelezwa kuwa lengo la mpango huo ni kuboresha jiji na kulitofautisha na halmashauri zingine    pamoja na utambuzi wa kimaeneo, mvuto wa mwonekano wa mitaa na kata.
“Hivyo, matumizi haya ni kwa kata zote 41 kulingana na rangi husika ya kupaulia au kupakwa. Mpango huu utafanyika katika maeneo yote ambayo aidha vibali vya ujenzi vimeshatolewa au kwa maeneo ambayo hayana vibali vya ujenzi,” anasema Kunambi.