Dodoma mpya na viwanja maarufu vya starehe

Muktasari:

Kwa wale ambao wanapenda starehe hutafuta maeneo ya starehe ili kupata viburudisho mbalimbali na ni kawaida kwa wasafiri wanaokwenda maeneo mapya kwa wale ambao wanapenda starehe, kuuliza kwa wenyeji ni wapi pa zuri pa kuweza kufurahi.

Dar es Salaam. Kila mtu anapokwenda katika eneo au mkoa fulani anapenda kutafuta sehemu ya kuburudika au kufanya kile anachopenda.

Kwa wale ambao wanapenda starehe hutafuta maeneo ya starehe ili kupata viburudisho mbalimbali na ni kawaida kwa wasafiri wanaokwenda maeneo mapya kwa wale ambao wanapenda starehe, kuuliza kwa wenyeji ni wapi pa zuri pa kuweza kufurahi.

Kwa Jiji la Dodoma mambo yanaendelea kubadilika kadri siku zinavyokwenda. Wiki iliyopita nilikuwa mjini humo ambako nilikuwa sijaenda kwa muda wa miezi sita iliyopita. Kwa wale ambao wamekuwa wakienda Dodoma mara kwa mara watakubaliana nami kuwa maeneo ya starehe yameongezeka katika jiji hilo.

Pamoja na mengine kufungwa, kuna mapya yamefunguliwa na yanavutia na kulifanya jiji hilo liwe la burudani siku za mwisho wa wiki na siyo tu mwisho wa wiki, bali hata katikati lakini zaidi nyakati za jioni baada ya muda wa kazi

Kutokana na kituo kikuu cha mabasi Dodoma kilichokuwa katikati ya mji kuhamishiwa Viwanja vya Nanenane, kwa wageni ambao hawajawahi kufika Dodoma mjini wanaopenda starehe wanaweza wanapotoka kituoni hapo kuelekea mjini kuanzia Kisasa Park kupata burudani.

Hiki ni kiwanja kipya kwa wapenda starehe wanaopenda kuuliza kwamba kiwanja gani kina ‘kick’. Ni eneo unaloweza kupata starehe na burudani mbalimbali ukiwa jijini humo.

Eneo hilo lina mandhari nzuri ya kupata vinywaji na watoto kucheza, hivyo ni mahala unapoweza kwenda na familia kwa ajili ya watoto kucheza na wakubwa kupata vinywaji.

Mbali na hilo kuna ‘kiwanja’ kinaitwa Rainbow ambako napo ‘kunabamba’ ipasavyo. Ni kiwanja kilichopo katika njiapanda ya Area D jijini Dodoma ambacho pia ukiwa unatokea Kituo Kikuu cha Mabasi Dodoma unaweza ukaomba wenyeji wakupeleke.

Ni maeneo ambayo yameboreshwa na mengine kuanzishwa ili kuweza kuwaburudisha wakazi wapya wa jiji hilo hasa watumishi wa Serikali waliohamia mjini humo wengi wakitokea jijini Dar es Salaam ambako kuna viwanja vingi vya starehe.

Kuongezeka kwa maeneo ya starehe na burudani katika jiji hilo kumeelezwa na baadhi ya wakazi kuwa kutaongeza mzunguko wa fedha na pia kuwafanya wakazi wapya hasa watumishi wa Serikali wanaohamia wajione kuwa bado wapo jijini Dar es Salaam.

John Daud ambaye ni mkazi wa jiji hilo akiwa katika eneo la Rainbow ananiambia kuwa maisha ya Dodoma yanabadilika kadri siku zinavyokwenda. Anasema pamoja na kwamba mzunguko wa fedha umekuwa mgumu, lakini jiji linabadilika na maeneo ya burudani yanaongezeka huku vinywaji vikiuzwa kwa bei inayoridhisha.

“Wewe zamani ungekuta saa hizi watu wengi wako mnadani Msalato kwenye nyama, lakini si unaona watu wanavyokunywa hapa na wamejaa maana yake wamepata eneo jingine la kujiburudisha,” anasema huku akiinua glasi yake kwa ajili ya kuendelea kupata kinywaji.

Kwa wale ambao hawaijui Dodoma, Mnadani Msalato ni eneo maarufu ambalo huuzwa nyama choma na vinywaji mbalimbali kila Jumamosi. Eneo hilo siku hiyo hufurika wakazi wa Dodoma na wageni wakiwemo viongozi mbalimbali na wabunge hasa kipindi cha mikutano ya Bunge.

Pamoja na kwamba kituo kikuu cha mabasi kimehamia Nanenane kuna kampuni za mabasi kama Shabiby Line, Kimbinyiko na ABC ambazo zina ofisi zao karibu na katikati ya jiji na unaposhuka ukitokea Dar es Salaam na maeneo mengine unaweza ukaulizia kiwanja kilicho karibu kwa ajili ya starehe na burudani.

Chako ni Chako ni eneo maarufu sana kwa starehe jijini Dodoma na ndipo nilipofikia baada ya kushuka kwenye kituo cha mabasi cha ABC. Chako ni Chako ya sasa si ile ya zamani. Kuku zipo kama kawaida, lakini hivi sasa eneo la kupata vinywaji limeboreshwa zaidi.

Hapa nilikuta watu wakiwa wamekaa kwenye viti virefu na kuegemea kwenye meza ambazo ziko kama mfano wa mitumbwi, huku wakiangalia mubashara upokewaji wa ndege kubwa ya Serikali aina ya Dreamliner. Ni sehemu palipoboreshwa na penye burudani nzuri kwa wewe ambaye unataka kujiachia Dodoma.

Si hapo tu kwa karibu na kituo cha mabasi ya kampuni ya Kimbinyiko kuna Dodoma Canival, eneo jingine la muda mrefu kidogo, lakini ni kiwanja kizuri kwa burudani na chakula. Kwa hiyo ukitaka utoke vipi Dodoma unaweza ukaanzia hapo pia.

Serikali kuibuka na kiwanja kipya

Pamoja na kwamba kuna maeneo hayo kadhaa na mengine ambayo nitaendelea kukutajia ili usisumbuke uwapo Dodoma, mkurugenzi mtendaji wa Jiji la Dodoma, Godwin Kunambi anasema bado kuna mahitaji ya maeneo ya burudani, bustani za wanyama na viwanja vya michezo.

Kutokana na mahitaji hayo anasema, “tunajenga eneo la burudani pale Chinangali kuwe na swimming pool, table tennis, eneo la watu kupumzikia, hivyo mwakani mwezi wa kumi watu watakuwa wanafurahi hapo.”

Anasema wanafanya hivyo kwa kuwa wamegundua mwisho wa wiki watu wengi wanakwenda Dar es Salaam kwa ajili ya burudani, hivyo wanataka wawe wanabaki Dodoma.

Katika maeneo ya burudani bado kuna kama Rose Garden ambayo ipo muda mrefu na imeendelea kuwepo ikitoa burudani na chakula kwa wageni na wenyeji. Pia klabu za usiku kama 84 nazo zimeendelea kuwepo na kuwaweka wakazi wapya wa jiji hilo katika maisha ya furaha muda wote.

Kwa mtazamo huu wa baadhi tu ya maeneo ya kustarehe jijini Dodoma pamoja na kwamba yako mengi unaweza ukaingia sehemu yoyote unayoona itakayokufurahisha na kuweza kufurahia kukua kwa Jiji la Dodoma kulikochagizwa na kuhamia kwa Serikali jijini humo.