Dodoma waongeza muda wa kulipia viwanja

Muktasari:

Badala ya mwezi mmoja wa awali, sasa ni miezi mitatu


Dodoma. Halmashauri ya Jiji la Dodoma imeongeza muda wa kulipia viwanja kutoka mwezi mmoja wa awali hadi miezi mitatu.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Ijumaa Mei 25, 2018 mkurugenzi wa jiji hilo, Godwin Kunambi amesema wameamua kuongeza muda huo baada ya kusikiliza maoni ya watu wengi waliotaka muda kuongezwa.
Awali, wakati akitangazwa kuanza kuuzwa kwa viwanja vya makazi, biashara na taasisi katika maeneo ya Mtumba na Iyumbu, halmashauri ilitoa muda mwezi mmoja tu kwa mtu atakayenunua kiwanja katika jiji hilo, kutakiwa awe amekamilisha malipo yote vinginevyo angenyang'anywa kiwanja.
" Tumeongeza muda wa kulipia viwanja kutoka mwezi mmoja wa awali hadi miezi mitatu tangu siku mtu alipopata hati ya malipo, nia yetu ni kumwezesha kila mwananchi amiliki kiwanja na kupata makazi bora," amesema Kunambi.
Ofisa Mipango Miji wa Jiji la Dodoma, Joseph Mafuru amesema kuongezwa kwa muda wa kulipiwa viwanja siyo sababu ya kuanza kujenga makazi holela na kuwatahadharisha wananchi  kujiepusha na ujenzi holela.