KUELEKEA DODOMA: Dodoma wasema walishajipanga

Mbunge wa jimbo la Dodoma Mjini ambaye ni Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana na Ajira Anthony Mavunde

Muktasari:

Wakizungumza na gazeti hili jana katika kikao cha Baraza la Madiwani, wabunge na Mkuu wa Wilaya Christina Mndeme walisema kila kitu kipo vizuri.

Dodoma.Viongozi wa Manispaa ya Dodoma wamejigamba wana uwezo wa kupokea makao makuu ya nchi, kwani walishajipanga.

Wakizungumza na gazeti hili jana katika kikao cha Baraza la Madiwani, wabunge na Mkuu wa Wilaya Christina Mndeme walisema kila kitu kipo vizuri.

Mbunge wa jimbo la Dodoma Mjini ambaye ni Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana na Ajira Anthony Mavunde, alisema ujio wa makao makuu ni jambo la heri kuliko vitu vingine.

Licha ya kukiri kuwa kila jambo lazima liwe na changamoto zake, alisema faida ya makao makuu ni kubwa ukilinganisha na hasara zake kwa jamii.

Mavunde aliwataka wakazi wa Dodoma kutumia fursa zilizopo kwa ajili kujipatia maendeleo.

“Nasisitiza kuwa, tusaidiane katika kuwaandaa watu wetu kikamilifu pamoja ili waweze kuzichangamkia fursa zilizopo ambazo zitawawezesha kujiinua kiuchumi,” alisema Mavunde.

Mkuu wa Wilaya Christina Mndeme alijigamba kuwa ana uwezo wa kuyapokea makao makuu lakini akataka kila kiongozi katika wilaya yake abadilike.

Akizungumzia uwezo wake alisema atatumia kila mbinu na njia ya kushawishi wadau mbalimbali na pia atakuwa tayari kufanya kazi saa zote usiku na mchana bila ya kuchoka.

Mkuu huyo alisema atafanya kazi usiku na mchana, kuifikisha ndoto ya Serikali katika nafasi inayotarajiwa.

Mbunge wa Viti Maalumu, Felister Bura, alisema uwezo wa Dodoma kuwa makao makuu ni mkubwa na hata kufikia jiji inawezekana.

Bura alitolea mfano kuwa katika makusanyo ya mwaka huu, manispaa hiyo ilivuka malengo kwa kukusanya asilimia 105 ambayo haijawahi kutokea.

Mbunge huyo aliwataka madiwani na watumishi wengine kushirikiana na hasa wakazi wa vijiji vya Vikonje na Ihumwa ambako mji wa Serikali unajengwa.