Dogo Dee Anavyofuata nyayo za Aslay, Janjaro

Muktasari:

Jijini Mwanza, yupo msanii mdogo kiumri ambaye anafanya vizuri na kufahamika kitaifa kutokana na ‘kukomaa’ kwake katika gemu.

Zamani wasanii wenye umri mdogo walikuwa wachache kwani fani ya kuimba na kufokafoka ilitafsiriwa kuwa ya kihuni au muziki usiokuwa na maadili.

Hata hivyo, zama zimebadilika na kukubalika kwake kumewafanya wazazi wakubali watoto wao wajihusishe na muziki

Mfano ni Dogo Hamidu, Young D, Mr Blue, Dogo Janja na Aslay ambao waliwavutia watu wengi hususan mashabiki wa Bongo Fleva miaka kadhaa iliyopita. Baada yao kukua kiumri na kimuziki, wengine wanaendelea kujitokeza.

Jijini Mwanza, yupo msanii mdogo kiumri ambaye anafanya vizuri na kufahamika kitaifa kutokana na ‘kukomaa’ kwake katika gemu.

Anasema wazazi wake, ambao ni Joseph Sahani (Marehemu) na mama yake Valentina, kwa pamoja walimpa majina ya Andrew Joseph miaka 15 iliyopita.

Anafahamika sana kama Dogo Dee kwenye ulingo wa burudani ya muziki na ameanza muziki tangu akiwa na umri wa chini ya miaka kumi na hiyo ilikuwa japo mwaka 2009.

Dogo Dee, ambaye ni mtoto wa sita kati ya watoto saba, wawili wa kiume na tano wa kike ni yeye tu ambaye anafanya muziki na hili halijamtofautisha kimaadili na wenzake kwani hadi mama yake mzazi, amekuwa sehemu ya wahariri wa mashairi yake kabla ya kuingia studio.

“Ngoma yangu ya kwanza imetoka mwaka 2009 nilifanikiwa kutoa singo yangu niliyomshirikisha Ney wa Mitego kwa jina la Jiunge Nasi,” Dogo Dee.

Kinyume na matarajio ya wengi, Dogo Dee amekuzwa na wasanii wengi akiwemo mwimbaji wa Gospo, Goodluck Gozbet ambaye pia waliwahi kufanya ngoma ya pamoja iliyojulikana kama Wape Kidogo.

“Watu wengi hawafahamu kwamba Gozberth mbali na uimbajo,yule kaka ni fundi kwenye ala za muziki amewahi kutengenezea watu biti kali kali na zikafanikiwa kuhiti. Kwa hiyo, nami amekuwa msaada mkubwa katika kunisaidia kimuziki jama vile mawazo, ushauri na mambo mengine,” Dogo Dee.

Maskani

Mzaliwa huyu wa mtaa wa Mabatini jijini Mwanza, ambaye kwa mwaka huu yupo kidato cha tatu katika shule ya sekondari ya Mtoni jijini Mwanza anasema huu mwaka kwake utakuwa tofauti na kipindi chote ambacho amedumu kwenye sanaa.

“Nimeweka mipangilio mizuri kuhakikisha kwamba mashabiki wangu kamwe hawataboreka lakinini pia nalenga kutanua wigo zaidi katika anga za kimataifa,” Anasema.

Darasani na muziki

Anaweka wazi kwamba yeye kama yeye anajitambua na anafahamu fika kwamba maarifa ya darasani ni muhimu na wala hawezi kukata tamaa na mama yake mzazi, Valentina hawezi kumruhusu kuacha shule.

“Jumatatu hadi Ijumaa ni darasani ila wikendi nafanya mambo yangu kama vile kuandika mistari na mazoezi ya muziki kwa ujumla,” Dogo Dee.

Baadhi ya ngoma...

Wimbo wa Miaka Kumi aliyomshirikisha Kala Jeremiah, Jiunge Nasi, Mungu Nipe ni miongoni mwa nyingi ambazo anasema hazikufaulu sana kwenye kasi iliopo. Aidha Dogo anasema wimbo wake wa Wabana Riziki aliyomshirkisha msanii mwenzake kutoka Mwanza, Baraka Da Prince ni sehemu ya miradi yake anayojivunia kwa sasa.

“Kwa sasa nipo katika harakati za kutoa video ya wimbo wangu mpya ambao unaenda kwa jina la Chaka to Chaka ambao nimeurekodia kwa Mbudu The Boss jiijini Mwanza,” anasema anaeleza.

Changamoto

Kama wasanii wengine, Dogo Dee anaeleza kwamba kupata mtu mwaminifu wa kusimamia kazi zake imekuwa tatizo.

Inamlazimu kusafiri hadi Dar es Salaam ili kutafuta promo lakini pia sehemu maalum ya kukutana na wasanii wakubwa kwa ajili ya kubadilishana mawazo pia ni ishu kubwa.

“Kama unavyoona wasanii wengi wa Mwanza wanakimbilia Dar hivyo inakuwa changamoto kubwa kukutana na watu wenye mwelekeo moja hata katika kuboresha baadhi ya miradi yetu,” anasema Dogo Dee.

Wito

Miaka kumi na mitano ambayo Mungu amempa pumzi ya kuishi, amebaini kwamba ili kuendelea au kupiga hatua maishani ni lazima nidhamu ihusike.

“Wasanii tuheshimiane, tuchangamane bila ya kubaguana lakini pia tujitume sanjari na kumtanguliza Mungu mbele,” anahitimisha.