EALA kushughulikia kero kuu za EAC

Spika wa Bunge la Afrika Mashariki (Eala),Daniel Kidega

Muktasari:

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa bunge hilo jijini hapa amesema jukumu la bunge hilo ni kusimamia maslahi ya wananchi baada ya Mbunge Bernard Mulengani aliyetaka shughuli za bunge ziahirishwe kwaajili ya kujadili hoja mahususi chini ya kifungu 13(1) ya kanuni za bunge hilo.

Arusha.Spika wa Bunge la Afrika Mashariki(Eala),Daniel Kidega amesema bunge hilo litashughulikia kwa haraka mambo muhimu ambayo ni changamoto zinazoikabili Jumuiya ya Afrika Mashariki(EAC).

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa bunge hilo jijini hapa amesema jukumu la bunge hilo ni kusimamia maslahi ya wananchi baada ya Mbunge Bernard Mulengani aliyetaka shughuli za bunge ziahirishwe kwaajili ya kujadili hoja mahususi chini ya kifungu 13(1) ya kanuni za bunge hilo.

Baada ya mbunge huyo wa Uganda kuwasilisha hoja zake ambazo alidai zinakwamisha shughuli za Jumuiya ni pamoja na nafasi ya Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kutoka Rwanda kuchelewa kujazwa.

"Nimefatilia nimeona majukumu ambayo kikanuni yanatakiwa yafanywe na Naibu Katibu Mkuu huyo yanafanywa na watu wengine ambao hawana mamlaka ya kutekeleza wajibu huo,pia kuna watumishi wawili walioajiriwa bila kufuata taratibu za ajira,"amesema Mulengani

Amesema kumekua na changamoto zinazokwamisha ufanyaji wa biashara kati ya Burundi na Rwanda na watu kutoka eneo moja kwenda lingine katika nchini hizo mbili ambazo ni wanachama wa EAC ambao unahitaji kuingiliwa kwa haraka.