Ebola yarudi kwa kasi DRC

Dk Tedros Adhanom Ghebreyesus

Muktasari:

Wasiwasi umetanda katika maeneo mengi ya mashariki mwa DRC baada ya Wizara ya Afya kutangaza kugundulika kwa ugonjwa huo katika maeneo ya Beni.

Beni, DRC. Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) imetangaza kusambaa kwa ugonjwa wa ebola nchini humo.

Wasiwasi umetanda katika maeneo mengi ya mashariki mwa DRC baada ya Wizara ya Afya kutangaza kugundulika kwa ugonjwa huo katika maeneo ya Beni.

Serikali imetangaza hayo wiki moja baada ya Shirika la Afya Duniani (WHO) kuanika mafanikio na mwisho wa janga hilo nchini humo.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la BBC, Wizara ya Afya  nchini humo imetoa taarifa WHO kuwa, vipimo vinne kati ya sita vimekutwa na virusi vya ugonjwa jijini Kinshasa na bado vipimo vingine vinaendelea kufanyika.

Mkurugenzi wa WHO, Dk Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema ugonjwa huo ni tishio nchini humo, lakini uwazi na ukweli wa Serikali katika kutoa taarifa ndio njia ya kwanza ya kuweza kuutokomeza.

Amesema ni rahisi kuanza mara moja jitihada za kuzuia Ebola kwa sababu wametoka kupambana na tatizo hilo hilo, hivyo vifaa na wafanyakazi wako tayari.

Maambukizi makubwa yameonekana katika eneo la Mangina ambako ni kilomita 30 kutoka mjini Beni.

“Tatizo hili limetokea katika mazingira tofauti na yale tuliyokuwa tukifanya kazi mara ya kwanza katika eneo la Kaskazini Mashariki,” amesema DK Peter Salam, msaidizi wa Mkurugenzi wa WHO.