Elimu bure isiwe kisingizio wazazi kukwepa majukumu

Muktasari:

Hayo yameelezwa na kiongozi wa mbio za mwenge kitaifa, Charles Kabeho.

Kibaha.Kiongozi wa mbio za Mwenge Kitaifa, Charles Kabeho ameshauri wazazi kutotumia kigezo cha Serikali inayotoa elimu bila, kuacha kugharamia mahitaji mengine ya watoto wawapo shuleni.

Kabeho ametoa rai hiyo leo Julai 17, 2018 katika Halmashauri ya wilaya ya Kibaha mkoani Pwani wakati wa mbio za mwenge wa Uhuru.

Amesema jamii bado ina wajibu wa kuwapa huduma wanafunzi shuleni ikiwemo chakula na sio kuwashindisha njaa kwa kisingizio cha elimu bure.

Kabeho amesema Serikali imeamua kutoa elimu bila malipo shuleni lakini haijakataza wazazi na walezi kuendelea kuwahudumia watoto wao katika mahitaji mengine muhimu kama vile kuwanunulia wanafunzi sare za shule, viatu na vingine.

Amesema mambo mengine muhimu jamii inayopaswa kulitazama ni pamoja na kuhakikisha watoto wanapata chakula wawapo shuleni ili kuwawezesha kumudu vipindi vyote vya masomo darasani.

"Katika mpango wa elimu bila malipo wananchi wajitaidi kutimiza wajibu wao kwa kuwahudumia watoto wao huduma zile muhimu ikiwemo kuwanunulia sare za shule, madaftari na mahitaji mengine na kuhakikisha pia wanapata chakula shuleni," amesema Kabeho.

Awali, Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Assumpter Mshama akipokea mwenge huo amesema utatembelea miradi saba ya maendeleo yenye thamani ya Sh10.9 bilioni ambayo imewekewa mawe ya msingi, kuzinduliwa na kukaguliwa

Pia miradi mingine minne ni ile inayobeba ujumbe wa kudumu wa mbio za mwenge wa uhuru kitaifa ikiwamo  miradi ya afya, mapambano dhidi ya rushwa za dawa zakulevya, malaria na VVU/Ukimwi.