Eneo lililouzwa kinyemela larejeshwa serikalini

Muktasari:

Eneo hilo lenye ukubwa zaidi ya eka moja lililopo kiwanja namba 69/70 jirani la Soko la Kilombero, liliuzwa kwa Kampuni ya Emoil Marketing Ltd siku moja kabla ya kuvunjwa baraza la madiwani.

Arusha. Hatimaye Rais John Magufuli amelirejesha serikalini eneo  lililowahi kutumika kama kituo cha mabasi katika Jiji la Arusha, lililouzwa kinyemela na baadhi ya madiwani wa CCM na watendaji mwaka 2005.

Eneo hilo lenye ukubwa zaidi ya eka moja lililopo kiwanja namba 69/70 jirani la Soko la Kilombero, liliuzwa kwa Kampuni ya Emoil Marketing Ltd siku moja kabla ya kuvunjwa baraza la madiwani.

Uamuzi wa Serikali kulitwaa eneo hilo ulitangazwa juzi na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na kupokewa kwa  shangwe na mamia ya wananchi wa Arusha katika mkutano wa hadhara uliofanyika juzi Uwanja wa Sheikh Amri Abeid.

Majaliwa alisema madaraka ya kutwaa eneo kwa maslahi ya umma ni ya Rais, hivyo kuanzia juzi linarudi na halmashauri ya jiji iandae utaratibu wa kulifanyia tathmini kumlipa fidia aliyelinunua na kumtafutia eneo jingine akiomba.

 Alisema Serikali ya awamu ya tano, itaendelea kuwajali vijana na wananchi maskini na kuanzia sasa maeneo yanatwaliwa kiujanja na wahusika kukimbilia mahakamani yatarejeshwa kwa umma.

Waziri mkuu, alieleza kuwa waliouza eneo hilo wana bahati hawapo, lakini wangekuwapo serikalini hivi sasa wangechukuliwa hatua kali.

Uamuzi huo wa Serikali umekuja takriban miezi mitatu tangu, Mkuu wa mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo kutangaza kuunda kamati maalumu kuchunguza mchakato wa kuuzwa eneo hilo.

Habari zaidi soma gazeti la Mwananchi