Evans Aveva alazwa ICU Muhimbili

Muktasari:

  • Mashtaka yao ni pamoja na kughushi, kuwasilisha nyaraka ya uongo na utakatishaji wa Dola 300,000 za Marekani.

Dar es Salaam. Rais wa Klabu ya Simba, Evans Aveva amelazwa katika kitengo cha wagonjwa mahututi Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).

Hayo yameelezwa leo Machi 8 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri na wakili anayewatetea, Evodius Mtawala wakati kesi hiyo ilipotajwa mahakamani hapo.

“Mshtakiwa wa kwanza Aveva, tangu jana amelazwa katika kitengo cha wagonjwa mahututi hali yake siyo nzuri," ameeleza wakili Mtawala.

Hata hivyo, mwendesha mashtaka wa Takukuru, Leonard Swai naye ameliambia mahakama kuwa Aveva ni mgonjwa na kwamba upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.

Baada ya kutolewa kwa maelezo hayo, Mtawala ameiambia mahakama kuwa walizungumza na upande wa mashtaka wataeleza jalada la kesi hiyo bado lipo kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) na wameomba wapewe siku 14 ili waweze kueleza kitu.

Hakimu Mashauri ameiahirisha kesi hiyo hadi Machi 22, 2018.

Wakati kesi hiyo ikitajwa mahakamani hapo alikuwapo Godfrey Nyange maarufu Kaburu ambaye ni makamu wa rais wa Klabu ya Simba.

Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka matano ya  uhujumu uchumi ikiwamo kughushi, kuwasilisha nyaraka ya uongo na kutakatisha wa kiasi hicho cha fedha.

Washtakiwa hao wapo mahabusu kutokana na kukabiliwa na mashtaka ya utakatishaji fedha ambayo hayana dhamana kwa mujibu wa sheria.