Ewura yaomba wananchi kutoa maoni ya IPTL

Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa Ewura, Titus Kaguo 

Muktasari:

Akitoa ufafanuzi kuhusu suala hilo leo Ijumaa jijini hapa, Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa Ewura, Titus Kaguo amesema kuna baadhi ya watu wanapotosha umma kwamba tayari IPTL wameshapewa leseni ya kuiuzia umeme Tanesco.

Dar es Salaam. Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) imewataka wananchi kuwa wazalendo kwa kujitokeza kutoa maoni kuhusu dhamira ya Kampuni ya kufua umeme ya IPTL kuomba kuongezewa muda wa leseni yake ya kuiuzia Tanesco umeme.

Akitoa ufafanuzi kuhusu suala hilo leo Ijumaa jijini hapa, Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa Ewura, Titus Kaguo amesema kuna baadhi ya watu wanapotosha umma kwamba tayari IPTL wameshapewa leseni ya kuiuzia umeme Tanesco.

"Ewura tunapokea maoni ya wananchi kwa maandishi, kwa hiyo itakuwa ni jambo la kizalendo kwa wananchi kujitokeza na kutoa maoni ama kupinga IPTL au kuunga mkono ili itusaidie nasi kufanya uamuzi," amesema.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa Ewura, Edwin Kidifu amesema mchakato unaofanyika sasa ni wa kisheria na maoni ya wadau ndiyo yataamua IPTL ipewe leseni au laa!

Kidifu anasema IPTL imeomba kuongezewa muda wa leseni yake kwa sababu mkataba wake wa miaka 20 na Serikali wa utekelezaji wa mradi wa umeme unakwisha mwaka 2022.