Fahamu kwa undani mfumo wa umwagiliaji wa matone

Muktasari:

Ni lazima mkulima aangalie eneo lililo karibu, miundombinu inayopitika kuelekea kwenye shamba pamoja na usalama wa mazao yako.

Mkulima anahitaji vitu vingi ili kupata mazao bora na yenye faida.

Ni lazima mkulima aangalie eneo lililo karibu, miundombinu inayopitika kuelekea kwenye shamba pamoja na usalama wa mazao yako.

Pia pasiwe na magugu hatari; wadudu hatari kama panya na pia shamba hilo lisiwe na historia ya kuwa limelimwa zao fulani kwa muda mrefu bila kubadilishwa.

Pamoja na hayo yote, lakini maji ni suala muhimu sana katika kilimo.

Unapaswa kuchunguza mazingira ya jirani kama kuna kisima ili kujiridhisha maji yanapatikana na kama yanapatikana kwa umbali upi? Je wamepata maji yenye chumvi au la?

Mambo haya yatakusaidia kupata picha kamili kwa shamba lako kwa sababu upatikanaji wa maji yenye chumvi kali huleta athari kubwa sana katika baadhi ya mazao ya kilimo.

Hivyo basi uwe na maji kutoka mtoni, mferejini, bwawani, ziwani, kisimani yatahitajika kuyatumia vizuri ili kusaidia uzalishaji mzuri lakini pia kuokoa rasilimali pesa.

Maji yakitumika vyema utaokoa rasilimali pesa, utapata mazao mazuri sana lakini pia ukiwa na maji kama hutojua njia salama ya kuyatumia vizuri ujue kuwa utapoteza rasilimali pesa hiyo haitoshi umwagiliaji ukizidi hupelekea mmea kuathirika na kufa kwa siku za mwanzo kwa ugonjwa uitwao damping off.

Lakini pia mimea ikishazaa matunda kama maji yakitumika kupita kiasi husababisha tunda kupoteza ladha, kupasuka au kuoza kitako pia (Blossom end rot).

Hivyo basi kama mkulima unapaswa kujua njia sahihi ya utumiaji maji yako kama rasilimali muhimu sana katika kilimo. Na mada yetu ya leo tutaangalia mfumo wa kisasa wa umwagiliaji.

Mifumo ya Umwagiliaji

Katika kilimo zipo njia mbali mbali amabazo hutumiwa na wakulima katika umwagiliaji wa mazao yao. Njia hizo huwa tofauti tofauti sana baina ya wakulima kutokana na sababu zifuatazo:-

Mojawapo, ni rasilimali pesa ya mkulima, aina ya zao ambalo mkulima anahitaji kulima na maeneo ya mashamba ambayo wakulima wapo.

Sababu nyingine ni upatikanaji wa maji wa eneo husika, historia ya eneo husika kuhusiana na upatikanaji maji, elimu ya mifumo ya umwagiliaji wakulima waliyo nayo na faida na hasara ya mifumo husika.

Vingine ni miundombinu ya shamba au mwonekano wa shamba husika.

Hivyo basi mkulima huchagua mfumo wa umwagiliaji kutokana na sababu zilizotajwa hapo juu.

Faida ya muundo huu

1. Husaidia kuhifadhi maji kwani hutumika kwa ufanisi wa hali ya juu .

2. Huokoa rasiliamali pesa kwani maji hutumika kidogo

3. Husaidia kupunguza magugu kwani maji huenda kwenye mmea moja kwa moja

4. Huupa mmea kiwango maalumu cha maji kinachohitajika

5. Hupunguza magonjwa ya kata kiuno (Damping off) na kuoza kitako

6. Hufanikisha uwepo wa maji misimu yoote

7. Hupunguza rasilimali pesa ya vibarua

8. Husaidia matumizi ya mbolea ya maji (Liquid manure)

Hasara ya mfumo huu

1. Mfumo huu una gharama sana katikakuweka. Sio chini ya milioni tatu kwa kuwekewa.

2. Mfumo huu unahitaji utaalamu hasa katika matengenezo madogo madogo.

3. Mfumo huu haufanyi kazi hasa katika mazao ambayo nafasi kati ya mche na mche ni sm 30.

4. Mfumo huu huwa na changamoto kubwa sana hasa katika mashamba yenye mwinuko.

5. Katika maandalizi huwa na gharama kwa sababu mfumo huu huhitaji matuta yaliyoinuka mara nyingi

Makosa yanayofanywa na wengi

Makosa mengi hufanywa kwa wale ambao wanashindwa kupata faida ya miundo hii kwa sababu zifuatazo;-

1. Wengi huweka miundo mbinu pasi na kuwa na elimu ya miundo hii.

2. Wengi huweka miundo mbinu hii peke yao bila wataalamu

3. Wengi huwa hawadadisi aina ya udongo, aina ya mmea wanaohitaji kulima, ukuaji wa mmea uliopo shambani. Hivyo huachia maji kiasi kile kile kila siku hii ni makosa

4. Hawafanyi matengenezo hasa kuzibua mipira.

Utatuzi

Mkulima unapaswa kupata wataalamu ambao watakuja kupima shamba lako kwanza, kisha watachora ramani ya shamba na mwonekano husika wa miundo mbinu itakavyokuwa.

Baada ya hapo udongo utapimwa. Zao unalohitaji kulima litatambulika.

Kutokana na aina ya udongo, urefu wa mizizi wa zao husika na hatua ya ukuaji wa zao husika itasaidia kujua ni muda gani maalumu wa kumwagilia mmea wako bila kuleta madhara wala kupoteza rasilimali fedha.