Familia ya mpinzani yakana kukutwa na silaha hatari

Muktasari:

Ni Kamishna huyu huyo ambaye haraka haraka baada ya uvamizi wa Oktoba 8, alitoa taarifa kwenye vyombo vya habari akiuambia ulimwengu mzima kuwa wamegundua mabomu kwenye nyumba yangu.

Abia, Nigeria. Familia ya kiongozi anayedaiwa kuhamasisha jimbo kujitenga, Nnamdi Kanu imetupilia mbali madai yaliyotolewa na Kamishna wa Polisi wa Abia, Anthony Ogbizi kwamba jeshi hilo lilikamata silaha hatari kutoka makazi yake.

Kamishna huyo alitoa taarifa akisema walikamata silaha walipovamia makazi ya kiongozi huyo yaliyoko Afara Ukwu kwa ushirikiano na Jeshi Oktoba 8.

Lakini Emmanuel Kanu, msemaji wa familia hiyo amewaambia waandishi wa habari kwamba ikiwa kuna silaha zilikamatwa kwenye makazi ya ndugu yao basi zitakuwa zilitegeshwa na vyombo vya usalama.

Alimshutumu Ogbizi kwa kutunga hadithi ili kuhalalisha “uvamizi haramu” ili ionekane alikuwa akitekeleza majukumu yake, limesema gazeti la The Nation.

"Huyu Kamishna wa Polisi mpya ni mtu yuleyule aliyekuja nyumbani kwetu siku mbili baada ya uvamizi uliofanywa Septemba 14 akiwa na magari mawili aina ya Hilux na Prado SUV akavunja kibaraza cha kuegesha magari na akaharibu magari yaliyokuwa yameegeshwa.

"Ni Kamishna huyu huyo ambaye haraka haraka baada ya uvamizi wa Oktoba 8, alitoa taarifa kwenye vyombo vya habari  akiuambia ulimwengu mzima kuwa wamegundua mabomu kwenye nyumba yangu. Jeshi kwa upande mwingine lilikanusha likisema hakuna uvamizi uliofanyika kwamba halikuwahi kuja nyumbani kwangu.

"Nyumba ambayo haikuwa na mtu ndani ispokuwa mlinzi aliyepewa kazi ya kuitunza, ghafla waliivamia na ndipo wakaja na habari hiyo kwamba walikuta bunduki, bunduki ya mitutu miwili na bomu la petrol. Nani aliyetengeneza? Nani aliyeweka? Hayo ndiyo maswali ya kujiuliza."