Familia Mo Dewji yasitisha kuzungumza na vyombo vya habari, yaishukuru kampuni ya Mwananchi

Muktasari:

Familia ya mfanyabiashara maarufu Tanzania, Mohammed Dewji ‘Mo Dewji’ aliyepatikana leo  Jumamosi Oktoba 20, 2018 saa nane usiku ikiwa zimepita siku nane tangu alipotekwa,  imesema haitafanya mkutano na waandishi wa habari kama ilivyokuwa imepangwa awali


Dar es Salaam. Familia ya mfanyabiashara maarufu Tanzania, Mohammed Dewji ‘Mo Dewji’ aliyepatikana leo  Jumamosi Oktoba 20, 2018 saa nane usiku ikiwa zimepita siku nane tangu alipotekwa,  imesema haitafanya mkutano na waandishi wa habari kama ilivyokuwa imepangwa awali.

Akizungumza na MCL Digital leo, Gullam Dewji baba mzazi wa mfanyabiashara huyo amesema kwa sasa wana furaha, na mkutano huo hautafanyika leo.

Amesema angefurahi kama mwanaye angepewa muda wa kutulia na kuamua kipi cha kuzungumza, huku akibainisha kuwa hata yeye pia hakuwa akipumzika kutokana na juhudi alizokuwa akifanya kumtafuta Mo Dewji.

“Mkutano sidhani kama tutaweza kuufanya leo. Tungeomba  mtupe nafasi kidogo. Nafikiri tutawajulisha kama ilivyokuwa awali unajua Mohammed ametoka katika matatizo ni  vyema akapumzika na hata mimi sijalala unajua,” amesema Gullam.

"Hata hivyo nawashukuru sana  jinsi mlivyokuwa karibu nasi wakati wote huu wa hili tatizo. Tukitaka kuongea tutawapa taarifa.”

Gullam aliishukuru kampuni ya Mwananchi Communication’s Ltd (MCL) inayochapisha magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti kwa jinsi ilivyokuwa ikiripoti tukio la kutekwa kwa mfanyabiashara huyo, hadi kupatikana kwake.