Familia iliyosusa mwili mochwari yataka tume kuchunguza chanzo cha kifo

Muktasari:

Salum Kindamba aliuawa hivi karibuni eneo la Jet Lumo ikidaiwa ni kwa kupigwa risasi na polisi na mwili wake umehifadhiwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) tangu mwanzoni mwa wiki iliyopita.

Dar es Salaam. Familia iliyosusa kuchukua mwili wa ndugu yao uliopo mochwari, imetaka Serikali iunde tume kuchunguza mazingira ya kifo chake, vinginevyo wataendelea kuuacha huko.

Salum Kindamba aliuawa hivi karibuni eneo la Jet Lumo ikidaiwa ni kwa kupigwa risasi na polisi na mwili wake umehifadhiwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) tangu mwanzoni mwa wiki iliyopita.

Wakati familia ikisema hayo, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa amesema jeshi hilo linafanya kazi kwa kufuata utaratibu na kama wanaendelea kususia, mwili huo utaendelea kubaki mochwari.

“Kama wanasema hawatachukua mwili, basi utaendelea kubaki maana polisi tunafanya kazi kwa kufuata utaratibu na suala la uchunguzi linafanywa kwa msingi huohuo. Hakuna ubishi kuwa Salum aliuawa kwa risasi, kuhusu ripoti ya uchunguzi haitolewi na polisi kuna utaratibu wake,” alisema Kamanda Mambosasa.

Lakini Omary Kindamba ambaye ni kaka wa marehemu alisema jana kuwa ndugu yao aliuawa katika mazingira ya kutatanisha na juhudi za kupata ukweli wa jambo hilo kutoka Jeshi la Polisi zimeshindwa kuzaa matunda hivyo wanataka tume huru kuchunguza tukio hilo.

“Tunaambiwa ndugu yetu alikuwa jambazi, hilo hatukubaliani nalo ndiyo maana tunataka iundwe tume ichunguze jambo hili. Sisi tunawalalamikia polisi, ili kuondoa wingu lazima iwepo tume huru ambayo itaeleza ukweli wa mambo baada ya kuhoji pande zote,” alisema.

Omary alisema wanatambua ndugu yao hajawahi kujihusisha na matukio ya kutiliwa shaka na hata sehemu alikokuwa akifanya kazi rekodi zake zinaonyesha alikuwa mwadilifu na mtu wa kujituma.

Alisema madai kuwa ndugu yao alikuwa jambazi si tu yameipaka tope familia yao lakini inawaweka kwenye mazingira magumu watoto wake ambao bado ni wanafunzi wa shule ya msingi.

“Hatutaki fedha kwa kuwa hatuwezi kurejesha uhai wa ndugu yetu. Tunataka tume ichunguze ili iusafishe ukoo wetu maana tumepakwa tope na hata hawa watoto aliowaacha marehemu watasoma kwa shida, wakienda shuleni wataambiwa ni watoto wa jambazi, hilo hatulitaki na tunasisitiza kuendelea na mgomo wetu wa kutochukua mwili wa marehemu hadi pale ukweli utakapofichuliwa,” alisema.

Alisema familia inalalamikia ripoti ya Muhimbili kuhusu chanzo cha kifo cha ndugu yao wanayedai alipigwa risasi Agosti 11 akiwa Jet Lumo na marafiki zake watatu.

Watatu hao wanashikiliwa na polisi katika Kituo cha Chang’ombe na kwa mujibu wa kaka wa marehemu wanakabiliwa na kosa la kujeruhi.

“Kesho (leo) tutakwenda tena polisi Chang’ombe kufuatilia suala hili na kuona kama tutapatiwa ripoti ya uchunguzi kuhusu kifo chake. Tulipokwenda (juzi) jana tuliambiwa turudi kesho wakidai ripoti ilikuwa bado iko Muhimbili.”

Akizungumzia ripoti ya uchunguzi huo, Mkuu wa Kitengo cha Uchunguzi Muhimbili, Dk Praxeda Ogweyo alisema juzi kuwa inaonyesha alifariki kutokana na mshtuko uliosababishwa na kuvuja damu nyingi kwa sababu ya majeraha ya risasi.

“Ripoti ya postmortem (uchunguzi wa mwili wa marehemu) iliyoandikwa kwenye form ya polisi MFL.1 inaonyesha matokeo ya vitu vyote alivyoona mchunguzi kwenye mwili wa marehemu ambavyo hatuwezi kuviweka hadharani au gazetini,” alisema.