Familia ya Mzee Majuto yamweka kiporo mke wake

Muktasari:

Katika maelezo yake mama huyo wa watoto wanne, amesema ndugu hao walimwambia kwamba ataishi kwa fedha za pole ambazo waombolezaji mbalimbali wameendelea kumpa.

Dar es Salaam. Siku chache baada ya mke wa marehemu Mzee Majuto, Aisha Yusufu kudai kufukuzwa na familia ya msanii huyo, ndugu wametoa msimamo wao kuhusiana na sakata hilo wakisema wamezisikia tuhuma hizo.

Madai hayo yanakuja ikiwa ni siku 15 zimepita tangu alipofariki msanii huyo maarufu wa vichekesho aliyewahi kutamba na filamu kama Back From New York, Inye na Mzee wa Chabo.

Wiki iliyopita mwanamke huyo alizungumza na vyombo vya habari akidai kwamba baada ya kumalizika kwa shughuli za maziko, ndugu walimwambia aanze kujitegemea kwa kila kitu ikiwemo chakula, jambo ambalo alilitafsiri ni sawa na wamemfukuza.

Katika maelezo yake mama huyo wa watoto wanne, amesema ndugu hao walimwambia kwamba ataishi kwa fedha za pole ambazo waombolezaji mbalimbali wameendelea kumpa.

MCL Digital ilizungumza na Hamza ambaye ni mtoto wa kwanza wa Mzee Majuto kwa njia ya simu, ambaye alisema hayupo tayari kuongea kwa sasa hivi lolote juu ya suala hilo mpaka hapo itakapofika siku ya kufanya arobaini.

“Arobaini ni Septemba 15 mwaka huu, wewe naomba uje huku Tanga Septemba 14 tutaongea kwa kirefu na utajua kwamba tulimfukuza au la ila kwa sasa siwezi kukuambia lolote kuhusu jambo hilo,” amesema msimamizi huyo wa familia.

Kwa upande wake mtoto wa tano wa Majuto, Abuu Athuman, amesema anachojua mama yao amekwenda Dar es Salaam baada ya kukosekana kwa watu wa kukaa naye katika kipindi chote cha eda kwa kuwa wengi wana shughuli zao.

Pia amesema kwamba vyakula vipo vya kutosha tangu kulipotokea msiba na tuhuma za mama huyo kwamba amefukuzwa sio za kweli kwani hawawezi kufanya hivyo kwa kuwa wanamtambua kama mama yao.

“Yule ni mama yetu, hatuwezi kumfukuza isitoshe ana watoto wadogo ambao tunatakiwa tuhakikishe wanalelewa kama enzi baba alivyokuwa hai ikiwemo kusoma.” Naye mke wa Majuto alipotafutwa, amesema kwa sasa familia yake imemkataza kuzungumza na vyombo vya habari na kusisitiza alichokisema awali ndio ukweli wenyewe.

Nasra Abdallah