Familia ya mfanyabiashara Mo Dewji : Hatujapata taarifa mpya

Azim Dewji msemaji wa familia ya Gulam Hussein Dewji akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusu tukio la kutekwa kwa Mohammed Dewji. Kushoto ni Gulam Hussein ambaye ni baba mzazi wa Mo. Picha na Maktaba

Muktasari:

  • Familia ya mfanyabiashara huyo aliyetimiza siku saba leo tangu alipotekwa Alhamisi iliyopita imesema bado inawaomba Watanzania waendelee kumuombea ndugu yao apatikane akiwa salama






Dar es Salaam. Familia ya Gulam Hussein Dewji imesema haijapokea taarifa yoyote yenye kutia matumaini ya kupatikana kwa mtoto wao Mohammed Dewji (43).

Familia hiyo juzi ilitangaza donge nono la Sh1 bilioni kwa atakayetoa taarifa zitakazosaidia kupatikana kwa bilionea huyo kijana.

Leo, Mo Dewji anatimiza siku ya nane tangu alipotekwa alfajiri ya Alhamisi iliyopita katika Hoteli ya Colosseum iliyopo Oysterbay jijini Dar es Salaam alikokwenda kufanya mazoezi.

Polisi wamesema pamoja na mambo mengine kuwa utekaji wa mfanyabiashara huyo mwenye ushawishi mkubwa kwa jumuiya ya wafanyabiashara nchini ulitekelezwa na Wazungu wawili.

Kufuatia tukio hilo, familia yake ilianza kushirikiana kwa karibu na vyombo vya usalama kumsaka bila kutoa neno, lakini siku nne baadaye iliamua kujitokeza hadharani na kutangaza dau la Sh1 bilioni kwa atakayetoa taarifa zitakazowezesha kupatikana kwa kijana wao.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa hivi karibuni aliliambia Shirika la Habari la Ujerumani kuwa kuna dalili watekaji hao walifanya hivyo kushinikizia wapewe fedha na si suala la kisasi.

Pamoja na hayo yote, bado familia inasema haijapokea taarifa inayotoa fununu yoyote ni wapi ndugu yao alipo.

“Hakuna tulichopata mpaka sasa ndugu yangu, familia bado tupo katika kipindi kigumu sana, nafikiri mzidi kutuombea jamani,” alisema Azim Dewji, ambaye ni msemaji wa familia hiyo.

“Samahani sana, nisingependa kulizungumzia hili mpaka nikae na familia. Baada ya hapo tunaweza kukutana na ninyi wiki ijayo labda tunaweza kuwaeleza kitu.”

Polisi wanadai kuwa Mo Dewji alitekwa na Wazungu wawili katika tukio ambalo lilihusisha magari mawili, jingine likiwa ndani na jingine nje ya uzio wa hoteli hiyo.

Kwa upande mwingine, dereva wa Uber aliyedai kushuhudia tukio hilo alipozungumza na Mwananchi, alisema aliwaona watekaji wanne walioficha nyuso ambao walimnyakua Mo kutoka ndani ya hoteli na kumtoa nje kabla ya kupiga risasi juu na kutokomea naye.

Taarifa za kutekwa kwa mbunge huyo wa zamani wa Singida Mjini, mlezi na mwekezaji wa klabu ya Simba zilisambaa haraka katika mitandao ya kijamii na kusababisha mshituko kwa wananchi na jumuiya ya wafanyabiashara.

Ni kwa nini na nani amemteka Mo ?

Hiki kimeendelea kuwa kitendawili kikubwa si tu kwa familia, bali hata kwa mamlaka za uchunguzi nchini ikizingatiwa kuwa tajiri huyo hajawahi kuwa na rekodi ya ‘kukwanguana’ na watu kibiashara au kisiasa.

Kisiasa

Mo Dewji aligombea na kuchaguliwa kuwa mbunge wa Singida Mjini mwaka 2005 na kukitetea tena kiti chake 2010 kabla ya kuamua kutogombea nafasi hiyo katika Uchaguzi Mkuu wa 2015.

Tangu wakati huo, Mo Dewji aliamua kukaa mbali na siasa na amekuwa makini kutoa kauli za kuunga mkono au kupinga maoni ama kundi lolote la siasa, huku akitoa zaidi maoni ya kuhusu njia za kufanikiwa kibiashara, kusimamia biashara na hata kidini.

Kibiashara

Anamiliki zaidi ya kampuni 40 chini ya mwamvuli wa kampuni mama ya Mohammed Enterprises Tanzania Ltd (MeTL), zinazofanya biashara katika nchi kadhaa za Afrika zikiwamo Kenya, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Malawi, Zambia, Msumbiji na Sudan Kusini.

Biashara zake zinachangia asilimia 3.5 ya pato la Taifa na hapa Tanzania kampuni zake zinatoa ajira za moja kwa moja kwa zaidi wa watu 23,000.

Pia katika umri wa miaka 43, ametangazwa na Jarida la Forbes kuwa bilionea kijana kuliko wote Afrika akimiliki mali inayokadiriwa kuwa na thamani ya Sh3.5 trilioni.

Utajiri wake unatokana na kutawala sekta mbalimbali na kuliteka soko la bidhaa za walaji kama vile vyakula kiasi cha kushika namba moja kati ya kampuni binafsi zinazoongoza kwa kuajiri watu wengi. Haijawahi kuwapo tetesi au ripoti yoyote rasmi inayoonyesha kuwa shughuli zake za biashara zinaweza kumzalishia maadui kiasi cha kuamua kumteka.

Jana, Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola alirudia kuwaonya watu anaodai wanataka kujitafutia umaarufu wa kisiasa kupitia suala la kutekwa Mo, akisema Serikali haitawavumilia.

“Naomba tuviache vyombo vya dola vitekeleze majukumu yake na siyo kuanza kusambaza taarifa zinazomhusu mfanyabiashara huyu ambazo zinasababisha familia yake kupata simanzi zaidi,” alisema Lugola.

“Tutawafuatilia popote walipo ili kujua kwa nini wanasambaza. Mtanzania yeyote asithubutu, kwenye suala hili tuviache vyombo vya dola vifanye kazi yake ya kuendelea na uchunguzi.”

Hii ni mara ya pili kwa Lugola kutoa onyo hilo. Jumamosi iliyopita aliwaonya watu wanaotumia mitandao ya kijamii kusambaza taarifa zinazojenga hofu kwa Watanzania ikiwa ni pamoja na uchochezi pamoja na upotoshaji.

Katika tukio jingine jana, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Yusuf Masauni alikutana na watendaji wa wizara hiyo na ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalumu ya Zanzibar kujadili ufungaji kamera wa maalumu za kudhibiti na kuzuia uhalifu.

Katika kikao hicho kilichofanyika mjini Unguja Zanzibar, Masauni alisema Serikali inatambua umuhimu wa ulinzi na usalama kwa raia wake na iko katika mpango wa kufunga kamera hizo kwenye miji yote mikubwa nchini.

Alisema lengo la kufunga kamera hizo ni kuiwezesha Serikali kupambana na matukio ya uhalifu wa utekaji, makosa ya barabarani na uporaji wa fedha katika taasisi za fedha.

Mkutano huo umekuja kukiwa na maelezo kuwa kamera za usalama (CCTV) zilizofungwa katika Hoteli ya Colosseum hazionyeshi vizuri mtiririko wa tukio la kutekwa kwa mfanyabiashara huyo.

Hata hivyo, polisi wamekiri kutumia picha za kamera zilizofungwa jirani na jengo hilo kusaidia katika upelelezi unaoendelea wa tukio hilo.