Bariadi na mpango wa kuzalisha Chaki

Mwalimu akitumia chaki kuandika katika ubao

Muktasari:

Katika mkakati huo, Wilaya ya Maswa inatarajiwa kuendesha mradi mkubwa wa uzalishaji na usambazaji wa chaki katika shule zote mkoani humo na ziada itauzwa nje ya mkoa.

Bariadi. Mkoa wa Simiyu unakusudia kuanzisha mpango wa kila wilaya kuwa na mradi wa uzalishaji mali ambao siyo tu utatoa fursa kwa wananchi kuwekeza na kuimarika kiuchumi, bali pia utachangia pato na uchumi la wilaya husika, mkoa na Taifa.

Katika mkakati huo, Wilaya ya Maswa inatarajiwa kuendesha mradi mkubwa wa uzalishaji na usambazaji wa chaki katika shule zote mkoani humo na ziada itauzwa nje ya mkoa.

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Antony Mtaka alisema hayo wakati akizungumzia fursa na mikakati ya mkoa wake wakati wa semina maalumu ya Fursa inayoendeshwa na kampuni ya Clouds Media Group kwa kushirikiana na Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd  (MCL), iliyofanyika jana mjini Bariadi.

“Mradi huo utaingiza zaidi ya Sh300 milioni kwa mwaka ikiwa ni zaidi ya Sh25 milioni kwa mwezi iwapo chaki hizo zitasambazwa ndani ya Mkoa wa Simiyu pekee. Hii ni fursa ya kiuchumi na kibiashara inayohitaji kuchangamkiwa,” alisema Mtaka.