Fedha za Magufuli zapeleka ujumbe wa ‘moto’ vyama vya michezo

Muktasari:

Kauli ya Rais Magufuli imeibua hoja kuwa iwapo hivi sasa Serikali imeingia rasmi katika 'anga' la vyama vya michezo kukabiliana na ufisadi na matumizi mabaya ya fedha zinazotolewa

Dar es Salaam. Rais John Magufuli jana alikabidhi fedha taslimu Sh50 milioni kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), huku akiwatahadharisha kuwa wameingia mkataba wa moto.

Fedha hizo alizozikabidhi Ikulu jijini Dar es Salaam alipofanya mazungumzo na viongozi na wachezaji wa Timu ya Taifa (Taifa Stars), zimepeleka ujumbe kwa viongozi wa shirikisho hilo na vyama vya michezo kuwa ni kama Serikali imetia rasmi mguu katika vyama hivyo kwenye juhudi za mapambano dhidi ya ufisadi.

Katika mazungumzo yake na wachezaji pamoja na viongozi wa TFF, Rais aliwaambia viongozi hao kuwa ametoa fedha hizo kwa ajili ya kusaidia maandalizi ya Taifa Stars kwenye mechi ijayo ya kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika dhidi ya Lesotho.

Akizungumza kwa msisitizo, Rais Magufuli alisema hataki kusikia fedha hizo zinatafunwa na watu ambao hawaingii uwanjani, badala yake zitumike kwa maandalizi na akaonya viongozi wanaopenda kutumia mwanya wa timu kutafuna fedha.

“Wakati ninaingia madarakani nilikuta kuna viongozi kwenye sekta ya michezo wamekuwa majizi, wengine ni katika ngazi ya klabu nikasema hawa washughulikiwe. Sitaki kuzungumza sana hili kwa sababu wengine tayari wapo mahakamani wameshtakiwa,” alisema.

Aliongeza kuwa katika miaka ya hivi karibuni viongozi wengi wa michezo wamekuwa majizi akimaanisha wezi, ndiyo sababu hata Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), likaikatia Tanzania mgawo wa fedha za msaada ambazo hutolewa kwa nchi mbalimbali kusaidia maendeleo ya soka.

Katika makabidhiano hayo, Rais aliwaita kushuhudia Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe na Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Leodegar Tenga na nahodha msaidizi wa Taifa Stars, Erasto Nyoni.

Aliwatahadharisha viongozi wa TFF, BMT na wizara kuwa atatuma wakaguzi kwa kila senti anayoitoa na zile zitakazotolewa na wadau wengine ili kujiridhisha kuwa hakuna fedha inayopotea na wale watakaothubutu kuzila wajue watazitapika.

Pia aliagiza matumizi ya tiketi za kielektroniki katika viwanja vyote nchini ili kudhibiti mianya ya upotevu wa mapato na pia kuiwezesha Serikali kupata mapato stahiki kutokana na mgawo wake.

Rais alitumia nafasi hiyo kuziomba kampuni na watu mbalimbali kujitokeza kuisaidia timu hiyo iweze kufanikisha malengo ya kufuzu kwa ajili ya fainali hizo zitakazofanyika mwakani nchini Cameroon.

Alisema anataka ushindi katika mechi zote zilizobaki za kufuzu fainali ya Afrika.

Rais alionya kuhusu kuandaa sababu za kushindwa akisisitiza kuwa anachotaka ni ushindi na hataki kusikia visingizio vya hali ya hewa, hujuma au chochote bali timu itimize matarajio ya Watanzania wengi.

Alikemea tabia ya viongozi wengi kusafiri na timu akisema haiwezekani timu inapeleka wachezaji 15, lakini msafara unakuwa na viongozi 30 ambapo wengi wanaishia kwenda kulala hotelini kutwa nzima kwa kukosa kazi ya kufanya.