Fedha za jimbo zazua kizaazaa Zanzibar

Muktasari:

Mwakilishi adai wamepewa mara moja, waziri aahidi kutoa majibu Septemba; mwingine alilia uwekezaji

 Mwakilishi wa Shaurimoyo, Hamza Hassan Juma amesema kitendo cha Serikali kutowapatia wawakilishi fedha za jimbo kwa kipindi kirefu ni njia mojawapo inayokwamisha upelekaji wa maendeleo katika maeneo hayo.

Juma aliyasema hayo katika kikao cha Baraza la Wawakilishi kilichofanyika Chukwani nje kidogo ya Mji wa Zanzibar wakati akichangia ripoti ya Kamati ya Fedha, Biashara na Kilimo ya Baraza la Wawakilishi.

Alisema tangu walipochaguliwa mwaka 2015, wamepokea fedha za jimbo kwa awamu moja kiasi cha Sh20 milioni, lakini baada ya hapo hakuna fedha walizotumiwa na Serikali ili kuhudumia majimbo yao kama utaratibu ulivyo.

“Tunasikitika kuona wenzetu wabunge wanapata fedha kila kipindi, lakini sisi baada ya mara moja tu hakuna tena hadi leo. Hali hii inasikitisha na kurudisha nyuma maendeleo,” alisema Juma.

Alisisitiza kuwa kitendo hicho kimeanza kuleta sintofahamu majimboni kwa baadhi ya wananchi kutoamini kama wawakilishi wao bado hawajapatiwa fedha kwa ajili ya maendeleo ya Majimbo yao. Mwakilishi huyo aliomba Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango kuliangalia suala hilo na kufanya haraka ya kulipatia ufumbuzi kwa kuwapatia fedha ili lengo la kuwahudumia wananchi liweze kutimia.

Akichangia ripoti hiyo, pia Juma aliitaka Mamlaka ya Vitenga Uchumi Zanzibar (Zipa) kuharakisha utoaji wa vibali kwa wawekezaji ili miradi mingi ya maendeleo ifunguliwe.

Mwakilishi wa Paje, Jaku Hashim Ayoub alisema kitendo cha kucheleweshwa kwa vibali vya wawekezaji wa miradi mikubwa kinachelewesha uharakishaji wa maendeleo kwa wananchi.

Alisema umekuwapo usumbufu mkubwa kwa wawekezaji ambao huhangaishwa huku na kule serrikalini katika kushughulikia masuala yanayowahusu.

Mwakilishi huyo alisema kuwa kitendo hicho hakileti picha nzuri ya kustawisha miradi ya maendeleo kwa masilahi ya wananchi na Taifa. Jaku aliiomba Serikali kusimamia kwa umakini na kuhakikisha kuwa suala hilo linakoma mara moja kwa kuwa likipuuzwa linaweza kusababisha madhara makubwa ikiwemo wawekezaji ambao wana nia ya kuwekeza Zanzibar kukimbia kutokana na kuhangaishwa.

Waziri wa Fedha na Mipango Zanzibar, Dk Khalid Salum Mohamed alisema pamoja na maoni na vilio vingi vya wajumbe wa baraza hilo, taarifa kamili juu ya michango yao itatolewa Septemba kama ulivyo utaratibu wa Serikali.

“Kwa kuwa michango hii inatokana na taarifa ya kamati, basi utaratibu wetu ni uleule ifikapo mwezi wa tisa tutatoa taarifa kamili kwa yale yote mliyochangia ndani ya baraza hili kupitia ripoti hii ya fedha, biashara na kilimo,” alisema Dk Khalid.