Flyover ya Tazara kuanza kutumika Oktoba

Muktasari:

Awali ugeni huo wa waziri Moramotse ulianzia ziara yake Ofisi ya wakala wa barabara (Tanroads) mkoa wa Dar es Salaam kwa ajili ya kujifunza usimamiaji wa barabara za kitaifa

Dar es Salaam. Ujenzi wa barabara ya juu katika makutano ya barabara ya Mandela na Nyerere (Tazara) wenye thamani ya Sh95 bilioni unatarajia kukamilika  Mei na kutumika rasmi mwishoni mwa  Oktoba mwaka huu.

Hayo yamebainishwa leo Februari 6  wakati wa ziara ya Waziri wa ujenzi na usafirishaji wa Lesotho Lehlohonolo Moramotse ambaye yupo nchini  akiambatana na wataalamu wa wizara yake kwaajili ya kujifunza namna ambavyo wenzao wanasimamia ujenzi, ukarabati na utunzaji wa barabara.

Awali ugeni huo wa waziri Moramotse ulianzia ziara yake Ofisi ya wakala wa barabara (Tanroads) mkoa wa Dar es Salaam kwa ajili ya kujifunza usimamiaji wa barabara za kitaifa, kisha mradi wa mabasi yaendayo haraka (Dart) na baadaye kumaliza kwa kutembelea mradi wa  barabara ya juu ya Tazara.

Mkurugenzi wa Tanroads Mkoa wa Dar es Salaam mhandisi Patrick Mfugale amesema mradi wa ujenzi wa barabara hiyo yenye urefu wa mita 425 mpaka Mei utakuwa umekamilika kwa mambo yote mhimu lakini kuzinduliwa rasmi ni mwezi Oktoba.

Mshauri katika kampuni ya Kampuni ya Oriental Consultans Global na Eight Japan Engineering Consultants Kiyokazu Tsuji, ambao ndiyo wanaojenga mradi huo aliwaambia wageni hao kuwa mpaka mwishoni mwa Oktoba mradi huo utakuwa umekamilika.

"Mpaka sasa mradi umekamilika kwa asilimia 74.61 mipango ilikuwa mpaka Januari uwe umekamilika kwa asilimia 74.61, muda wa kazi mpaka sasa tangu kuanza Desemba 1 ni masaa 1,774,932 na hakuna  ajali hata moja ambayo imekwisha tokea," amesema   Tsuji.

 Kwa upande wake Waziri Moramotse alisema katika siku 3 za ziara yake iliyoanza Jumapili (Januari 4) amefurahia zaidi mradi wa Dart na wakirejea nyumbani kwao wataangalia namna ya kuanzisha.

" Katika jiji letu la Maseru kuna changamoto ya foleni, usafiri wetu wa mkubwa kule ni daladala, taksi na magari binafsi. Mradi huu utatufaa lakini sisi tutaweka maegesho ya magari ya kutosha ili watu waache magari yao hapo wakitaka kwenda mjini," amesema Moramotse