Furaha ya dhamana yaishia Takukuru

Muktasari:

Waliochiwa kwa dhamana na kuishia mikononi mwa Takukuru ni aliyekuwa Mhasibu wa Mkoa wa Kagera, Simbaufoo Swai ambaye ni mshtakiwa wa pili, aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Bukoba, Steven Makonda na Meneja wa Benki ya CRDB Tawi la Bukoba, Carlo Sendwa.

Bukoba. Furaha ya kuachiwa kwa dhamana kwa washtakiwa watatu kati ya wanne katika kesi ya kufungua akaunti feki ya tetemeko la ardhi, iliyeyuka muda mfupi baada ya kutiwa tena mbaroni na maofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).

Waliochiwa kwa dhamana na kuishia mikononi mwa Takukuru ni aliyekuwa Mhasibu wa Mkoa wa Kagera, Simbaufoo Swai ambaye ni mshtakiwa wa pili, aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Bukoba, Steven Makonda na Meneja wa Benki ya CRDB Tawi la Bukoba, Carlo Sendwa.

Maofisa wa Takukuru waliokuwa wametanda katika viunga vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Kagera, waliwakamata washtakiwa hao na kuondoka nao  baada ya kukamilisha taratibu za dhamana.

Akizungumza kwa simu jana, Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Kagera, Joseph Mwaiswelo alithibitisha kuwa taasisi hiyo inawashikilia lakini hakuwa tayari kuelezea tuhuma zinazowakabili.

Aliyekuwa Katibu Tawala Mkoa wa Kagera ambaye ni mshtakiwa wa kwanza katika kesi namba 239 ya 2016 inayowakabili washtakiwa hao, Amantius Msole, alirejeshwa rumande baada ya kutotimiza masharti ya dhamana.