Thursday, September 14, 2017

GGM yatoa tamko uharibifu wa bomba la maji

By Mwandishi Wetu, Mwananchi

Dar es Salaam. Menejimenti ya Mgodi wa Dhahabu Geita (GGM) imetoa taarifa kwa jamii kuwa hali ya usalama ndani ya eneo lake bado ni shwari.

Taarifa hiyo inatokana na vurugu zilizotokea leo zikihusisha madiwani wa halmashauri mbili za Wilaya ya Geita, ambao walifunga barabara ya kuingia mgodini.

Polisi walilazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya madiwani hao walioshirikiana na wananchi. Madiwani wawili wanashikiliwa na polisi.

“Tunatambua jitihada kubwa na nzuri inayofanywa na vyombo vya ulinzi na usalama kulinda watu waliokuwa wamekusanyika nje ya lango la kuingilia ndani ya eneo la mgodi asubuhi ya Septemba 14,” imesema taarifa ya mgodi huo kwa umma.

GGM imesema pamoja na jitihada za vyombo vya ulinzi na usalama kuzuia mkusanyiko huo bila kuleta madhara, wamebaini uharibifu wa bomba la maji ambalo miundombinu yake imegharimu fedha nyingi.

Mgodi huo umesema uharibifu wa bomba hilo linalotoa maji safi kutoka Ziwa Victoria kupitia Kijiji cha Nungwe hadi kituo cha usambazaji maji kwenye Bwawa la Nyankanga, utaathiri kwa kiwango kikubwa upatikanaji wa maji katika Mji wa Geita.

Katika kukabiliana na madhara ya jamii ya watu wa Geita kukosa maji baada ya uharibifu huo, GGM imesema ipo kwenye mchakato wa kufanya ukarabati wa bomba hilo haraka iwezekanavyo.

“Ukarabati utaanza pale tu vyombo vya ulinzi na usalama vitakapotuhakikishia usalama wa mafundi na vifaa wanavyovitumia,” imesema taarifa hiyo.

GGM imesema inaendelea kutoa ushirikiano kwa mamlaka husika kuhakikisha watuhumiwa wa tukio hilo wanafikishwa kwenye vyombo vya sheria.

“Tungependa kufanya shughuli zetu za kutekeleza miradi ya kuisaidia jamii ya Geita kwa hali ya usalama lakini pia kwa usalama wa wafanyakazi wetu,” imesema GGM.

Mgodi huo umesema utaendelea kushirikiana na Serikali na jamii inayozunguka eneo la mgodi ili kuharakisha urejeshaji wa maji na amani kwa jumla ndani ya mji wa Geita.

GGM imesema inaendelea kutathmini madhara na athari za hali ya sintofahamu inayoendelea ndani na nje ya mgodi.

-->