Gekul aibua bungeni sakata la taasisi ya Pride

Mbunge wa Babati Mjini,Pauline Gekul akiomba mwongozo wa Spika wakati wa mkutano wa 12 wa bunge unaondelea jijini Dodoma leo. Picha na Filbert Rweyemamu

Muktasari:

Inadaiwa kuwa viongozi wa Pride wamekimbia nchi na kuwatelekeza wafanyakazi zaidi ya 500 na wateja zaidi ya 150,000.

Dodoma. Mbunge wa Babati Mjini (Chadema) Pauline Gekul amemuomba Spika wa Bunge Job Ndugai kuagiza Serikali kutoa kauli kuhusu hali ya Shirika la Pride Tanzania.
Akiomba mwongozo wa Spika bungeni leo Septemba 13 2018, Gekul amesema kuna taarifa kuwa viongozi wa taasisi hiyo  ambayo Serikali iliwahi kuwa na hisa wamekimbia nchi na kuwatekeleza wafanyakazi na wateja wao.
Amesema wafanyakazi karibu 500 waliosambaa maeneo mbalimbali nchini hawajui hatma yao na wateja karibuni 150,000 hawajui watapataje haki zao.
Amesema tayari Rais na Waziri wa Fedha na Mipango Philip Mpango barua kuhusu malalamiko hayo hadi leo bado hajajibu.
“Naomba mwongozo wako kwanini Serikali isitoe kauli bungeni kuhusu hali ya shirika hili?”amehoji Gekul.
Baada ya maelezo hayo Ndugai amemtaka aseme mwongozo wake anaunganisha na swali gani na alipotaja swali aliloliunganisha alijijibiwa kuwa hakuna uhusiano.
“Hakuna uhusiano lakini Serikali imesikia,”amesema Ndugai.