Giggy ashindwa kuripoti kwa Waziri

Muktasari:

Waziri Shonza amesema ameshindwa kukutana na msanii huyo kama walivyopanga kutokana na matatizo ya kiafya lakini amesisitiza kuwa agizo lake lipo pale pale.

Mazungumzo kati ya Naibu Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Juliana Shonza na mwanamuziki Giggy Money kuhusu picha za nusu utupu na kufungiwa kujishughulisha na sanaa umekwama baada ya wote wawili kuugua.

Waziri Shonza amesema ameshindwa kukutana na msanii huyo kama walivyopanga kutokana na matatizo ya kiafya lakini amesisitiza kuwa agizo lake lipo pale pale.

Amesema alimwagiza msanii huyo afike ofisini kwake na kwamba atakutana naye pale hali yake kiafya itakapokaa sawa.

Kwa upande wake Giggy Money ambaye jina lake halisi ni Gift Stanford amesema ameshindwa kufika ofisini kwa Waziri huyo kutokana na matatizo ya kiafya yanayomkabili.

Giggy Money ambaye awali alifika Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) badala ya ofisini kwa Waziri huyo kama lilivyokuwa agizo, alisema alipanga kuonana naye wiki iliyopita lakini alishindwa kufanya hivyo kutokana na kusumbuliwa na maradhi ambayo hakuyaweka bayana.

Januari 8, Giggy Money alikimbilia Basata lakini aliambiwa ni vyema akaonana na Waziri aliyemuita kwa kuwa wao wapo chini ya Wizara yake.

Akitoa sababu ya kwenda Basata, msanii huyo alisema alishindwa siku hiyo kuonana na Waziri baada ya kutaarifiwa kuwa yupo safarini na angerejea Januari 15 hivyo kuamua kwenda Basata kwa ajili ya kupata ushauri zaidi ya nini cha kufanya.

Giggy Money na mwenzake Pretty Kind walifungiwa kujishughulisha na sanaa kwa muda wa miezi sita kutokana na madai kuwa wamekuwa wakifanya vitendo visivyoendana na maadili ikiwemo kuweka picha za nusu utupu katika mitandao ya kijamii.