Graca Machel apigilia msumari kauli ya Magufuli

Dodoma. Serikali imetakiwa kuongeza juhudi katika kukabiliana na wimbi la ongezeko la ndoa na mimba za utotoni linalokatisha ndoto za wasichana kielimu.

Wito huo umetolewa leo  na mwanaharakati maarufu wa haki za binadamu barani Afrika  Graca Machel wakati wa ziara maalumu ya kukagua miradi ya afya katika kijiji cha Mpamantwa wilaya ya Bahi mkoani Dodoma.

 Machel ambaye ni mjane wa mke wa rais  wa zamani wa Afrika ya Kusini Nelson Mandela pamoja aliwasili jana mjini Dodoma.

 Machel amesema inasikitisha sana kuona namna ambavyo maisha ya wasichana wadogo yanakatishwa na baadhi ya watu wazima wasiyokuwa na hofu ya Mungu ndani yao.

“Tanzania ni miongoni mwa nchi barani afrika ambazo zinakabiliana na changamoto kubwa ya ndoa za utotoni ambazo kwa kiasi kikubwa zinawanyima wasichana haki zao za msingi za kikatiba na kibinadamu,” alieleza.

Machel amewataka viongozi wa umma katika ngazi zote kushirikiana kwa karibu na viongozi wa mila na dini ili kupiga vita vitendo hivyo vya kikatili dhidi ya wasichana wadogo hapa nchini.

“Wasichana wanahaki ya kupata elimu, angalau ya kidato cha nne halafu ndiyo wawe katika nafasi nzuri ya upevu wa akili wa kuchagua hatma zao za ndoa na maisha mengine,” ameongeza na kuonya kuwa jitihada za seikali ya awamu ya tano ya Rais John Magufuli ya kutoa elimu bure haitazaa matunda tarajiwa kama janga hilo halitakomeshwa.

Kuhusu sekta ya afya,  Machel amesema pamoja na jitihada kubwa zilizoonyeshwa na Rais  Magufuli katika kuboreshwa huduma za afya hapa nchini, Tanzania bado inakabiliwa na changamoto nyingi za afya.

Kwa upande wake, Waziri wa afya Ummy Mwalimu amesema kuwa watanzania wengi bado hawatumii huduma za bima za afya zinazotolewa hapa nchini na hivyo kujikuta katika wakati mgumu wa kumiliki gharama za matibabu.

Pamoja na Serikali ya awamu ya tano kupunguza gharama za madawa kwa kiasi kikubwa, Waziri Mwalimu alisema sekta ya afya hapa nchii bado inakabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo ufinyu wa bajeti, upungufu wa wauhudumu wa afya pamoja na vifaa tiba muhimu, hasa katika maeneo ya vijijini.

“Hadi sasa, ni asilimia 28 tu ya watanzania ndiyo wanaotumia huduma za bima za afya, wakati lengo la serikali ni huhakikisha kwamba ifikapo Mwaka 2025, zaidi ya asilimia 70 ya watanzania wawe wamejiunga na mifuko mbalimbali ya bima za afya.