Friday, September 14, 2018

Guninita kuzikwa Septemba 19

 

By Tumaini Msowoya, Mwananchi tmsowoya@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mwili wa Mwenyekiti wa zamani wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, John Guninita unatarajiwa kuzikwa Jumatano Septemba 19, 2018 kijijini kwao Kibaoni, Ifakara mkoani Morogoro.

Guninita ambaye jina lake linabaki katika orodha ya wanasiasa wenye uwezo wa kutenda kile wanachoamini alifariki dunia jana Septemba 13, 2018 katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) alikokuwa akipatiwa matibabu.

Aizungumza na MCL Digital mdogo wa marehemu,  Gerald Guninita amesema mwili wa kaka yake utachukuliwa MNH Jumanne  asubuhi, misa ya mazishi itakayofanyika nyumbani kwake Tabata Kimanga.

Amesema, awali Guninita alikuwa anasumbuliwa na kwiwi, kiungulia na baada ya vipimo alibainika kuwa na uvimbe tumboni.

"Nitumie nafasi hii kushukuru kila aliyeshiriki kuokoa uhai wa kaka yangu wakiwamo madaktari wa Muhimbili, Bwana ametoa na Bwana ametwaa jina lake lihimidiwe," amesema.

Amesema pia wamepata salamu za rambirambi kutoka kwa Rais rais mstaafu, Jakaya Kikwete ambaye alikwenda kumjulia hali Guninita kwa zaidi ya mara nne alipokuwa amelazwa.

“Jana Jakaya amenipigiabsimu na ameniambia yupo nje ya nchi, lakini alikuwa akimtembelea mgonjwa mara kwa mara tunawashukuru," amesema.

Gerald amesema wameshafanya mawasiliano na viongozi wa CCM wa Ifakara kwa ajili ya mazishi na kwamba Guninita atazikwa kwa heshima za chama hicho.

-->